Mshahara Zanzibar juu kwa 100%


Salha Mohamed na Asha Kigundula
Dk Ali Mohammed Shein

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imetangaza nyongeza ya mishahara kwa asilimia 100 kwa watumishi wa umma ikieleza itaanza kulipwa Aprili.

Akihutubia maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar jana, Rais wa Visiwa hivyo, Dk Ali Mohammed Shein alisema mshahara kwa watumishi wa umma umeongezeka ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo.

“Katika kipindi hiki mipango yote imekamilika ya kulipa wafanyakazi wa Serikali kima cha chini cha mshahara kutoka Sh150,000 za sasa hadi Sh 300,000 kwa mwezi,” alisema.

Alisema katika miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Serikali imedhamiria kupandisha kiwango cha mshahara kwa watumishi wake.

Alisema uwajibikaji wa wafanyakazi kazini umeongezeka ingawa bado wapo wanaofanya kazi kwa mazoea ambao Serikali itaendelea kuwachukulia hatua za ziada ya kusimamia nidhamu kazini.

“Wapo watumishi walioondolewa kwenye dhamana ya kazi, wapo waliosimamishwa kazi kutokana na ubadhirifu wa fedha za umma na wapo wanaoendelea kuchunguzwa na taasisi husika,” alisema.

Dk Shein alisema Serikali imeendelea kusimamia na kudhibiti matumizi ya fedha kwa safari za nje na za ndani bila kuathiri kazi.

Alisema mafanikio yaliyopatikana katika maiaka 53 ya Mapinduzi ni mengi.

“Leo (jana) ni siku muhimu kwa historia ya Zanzibar ambapo miaka 53 iliyopita tulikata minyororo ya Wakoloni, wananchi walikataa kwa vitendo kudharauliwa, kunyanyaswa, kubaguliwa na kutoheshimiwa,” alisema.

Alisema Mapinduzi yalileta uhuru wa kweli na kusimamisha utawala wa Wakoloni katika misingi ya haki na maendeleo, wananchi wa Zanzibar waliporudisha heshima yao.

“Siku zote tutawakumbuka, kuwaenzi na kuwaombea dua waliojitoa mhanga kutukomboa, tuko huru na tunasherehekea mafanikio hayo,” alisema.

Alisema Serikali inaahidi kuendelea kuyaenzi Mapinduzi na kusherehekea kwa amani, umoja na mshikamano.

“Yapo mambo yanatekelezwa kwa mafanikio ikiwamo miradi 51 iliyowekwa mawe ya msingi kwenye halmashauri na ni haki ya kila mmoja kujivunia na kuendeleza mafanikio haya,” alisema.

Alisema mwaka wa kwanza wa kipindi cha pili cha awamu ya saba, Serikali ilianza vema utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 na dira ya maendeleo kwa mafanikio.

“Katika kipindi hiki mafanikio makubwa tuliyopata ni kuimarika kwa uchumi wetu, pato halisi la taifa limekua kwa kiwango cha wastani wa asilimia 6.6,” alisema.

Alisema pato la mtu binafsi limefika wastani wa Sh milioni 1.6 sawa na dola 817 mwaka juzi.

Alisema mwaka jana kasi ya mfumuko wa bei wa bidhaa na huduma ilifikia asilimia 6.7 ambapo kasi hiyo ilikua kwa asilimia 5.7 mwaka juzi.

“Mfumuko wa bei bado umedhibitiwa katika kiwango cha tarakimu moja. Mafanikio haya ni kutokana na jitihada za kukusanya mapato katika vyanzo mbalimbali,” alisema.

Alisema katika kipindi cha Januari hadi Novemba mwaka jana mapato yalikusanywa kutoka vyanzo vya ndani yakiongezeka kutoka Sh bilioni 336.6 mwaka juzi hadi sh bilioni 441.3 mwaka huu, sawa na ongezeko la asilimia 31.

Alisema Serikali ilipokea Sh bilioni 54.53 kutoka kwa washirika wa maendeleo kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka jana.

“Serikali ilitumia Sh bilioni 436.6 kati ya Januari na Oktoba mwaka jana, kwa jumla katika kipindi hicho mapato ya Serikali yalipindukia matumizi ya jumla ya Sh bilioni 4.7 sawa na ongezeko la asilimia mbili,” alisema na kuongeza kuwa Serikali inatarajia kununua meli mpya mwaka huu.

Makamu wa pili wa Rais, Balozi Seif Khalid alimpongeza Rais Shein kwa uongozi wa heshima na busara.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa miongoni mwa viongozi wengine na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hasan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, marais wastaafu, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Jakaya Kikwete, Benjamin Mkapa na Amani Abeid Karume.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo