Mery Kitosio, Arusha
IDADI ya wanaume wanaolalamika kuonewa
na wenzao mkoani hapa imeongezeka kutoka walalamikaji 34 mwaka 2015 hadi
kufikia 63 mwaka 2016 sawa na asilimia 48.
Akitoa taarifa hiyo ofisini kwake jana
Mkuu wa Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto wa Mkoa, Mkaguzi wa Polisi Happiness
Temu alisema idadi hiyo imeongezeka hivyo kuonekana kuwa wanaume nao wanafanyiwa
ukatili mkubwa na si wanawake peke yao.
Alisema ongezeko hilo lilitokana na
kuenea kwa elimu inayotolewa na askari wa Dawati kwa watu wa jinsia zote kupitia
vyombo vya habari hasa redio za hapa kwani hapo awali wanaume waliogopa
kujitokeza kulalamika haswa wanapoonewa ndani ya ndoa zao.
Alifafanua kuwa wengi wa wanaume hao
hufanyiwa ukatili wa kisaikolojia ambapo baadhi ya wenzao wanaonekana
kutowathamini huku wengine wakikataa kushiriki tendo la ndoa, hali ambayo hufanya
wanaume kujiona hawana uhalali wa kuishi na wenza wao.
“Mbali na ukatili wa kisaikolojia, pia
baadhi yao hufanyiwa ukatili wa kiuchumi ambapo baadhi ya wanawake wenye uwezo
kuzidi waume zao wakati mwingine hutoa uamuzi wa kifamilia pengine ukawa na
maendeleo, lakini bila kushirikisha wenzi wao hali inayowafanya wabaini kwamba inatokana
na kuzidiwa kipato na kushindwa kutengua uamuzi au kutoa ushauri,” alisema.
Alitaja wilaya inayoongoza kwa idadi ya
wanaume kulalamika katika ofisi yake kuwa ni Arusha iliyokuwa na walalamikaji
48, Arumeru wanane na Ngorongoro watatu. Wilaya ya Longido ina wawili huku
Karatu na Monduli zilikuwa mlalamikaji mmoja mmoja.
Alitoa mwito kwa viongozi wa kata,
mitaa, vijiji na vitongoji kuiarifu ofisi yake wanapokuwa na vikao maeneo yao
wazidi kusambaza elimu ya ukatili wa kijinsia kwa wanandoa, kwani wanaume wengi
awali hawakuwa na ufahamu pia wanaweza kutoa malalamiko yao kupitia Dawati
hilo.
Hata hivyo ofisi ya Dawati la Jinsia na
Watoto mkoa wa Arusha mwishoni mwa mwaka jana imekuwa ikitoa elimu ya ukatili
wa jinsia kwa wanafunzi wa shule za msingi zilizopo katika halmashauri ya Jiji
la Arusha ambazo ni Sombetini, Osunyai, Ngarenaro, Kaloleni, Burka na Elerai
hali ambayo imewasaidia wanafunzi hao kupata uelewa mkubwa juu ya ukatili.
0 comments:
Post a Comment