Frankius Cleophace, Tarime
WATUHUMIWA 10
waliokamatwa juzi wakihusishwa na tukio la kumcharaza viboko hadharani mwanamke
wameachwa huru na Jeshi la Polisi.
Watuhumiwa hao
waliachwa huru asubuhi ya jana baada ya kukaa rumande kwa siku mbili.
Hata hivyo, haijafahamika
sababu ya Polisi kuwaacha watuhumiwa hao kutokana na Kamanda wa Polisi wa Kanda
Maalumu ya Tarime/Rorya kushindwa kulizungumzia suala hilo hata alipotafutwa
ofisini kwake ambapo alidai ana kazi ambayo ilitakiwa kufanywa kwa wakati huo
na kushauri kuonwa kesho.
Baadhi ya wakazi
wa Rorya ambao ni Wasimbiti, walisema adhabu iliyotolewa kwao ni ya kawaida kwa
watu wenye tabia mbaya kwenye jamii yao.
Mwita Wambura wa
Nyamaguku alisema wazee hufikia kutoa adhabu kama hiyo kulingana na maelezo ya
mtuhumiwa.
"Ni kawaida
kwetu wazee wa Irienyi Ndodo kutoa adhabu kama hizo, maana kuna watu ni
wakarofi sana, lakini wazee wanasaidia kuwanyoosha na kurejesha maadili kwenye
jamii, na ndiyo maana hata aliyetendewa vile alishasahau na hakwenda kushitaki.
“Pia wazee
wanapotoa adhabu kama hiyo, huandika taarifa na sababu ya kufanya hivyo, hivyo
walikuwa sahihi," alisema Wambura.
Aliitaka Serikali
kuwapa nguvu wazee hao ili waendelee kusimamia maadili katika kabila lao, kwani
wakiacha kusimama kidete hali ya usalama itakuwa mbaya.
Hata hivyo, Rose
Mwita alipingana na msimamo wa Wambura kwa kudai kuwa haikuwa halali kutoa
adhabu kubwa kiasi kile hadi kumwacha uchi mama huyo mwenye umri wa miaka 38
mkazi wa kijiji cha Kinesi, Rorya.
Tukio la
kucharazwa viboko kwa mama huyo lilifanyika Januari 23 mwaka jana, lakini
lilikuja kufahamika Januari 9 mwaka huu baada ya kurushwa mitandaoni.
Hata hivyo,
kijana aliyerusha video hiyo kwenye mitandao ya kijamii, anakabiliwa na adhabu
ya wazee wa kimila ambao walisema alikiuka maadili ya kabila hilo.
Anaweza kutengwa
na jamii, kwa kipindi fulani asisalimiane nayo, au asinywe pombe kokote au kuchapwa
viboko.
0 comments:
Post a Comment