Suleiman Msuya
Jaji Joseph Warioba |
MAWAZI wakuu waliopata kuingia kwenye
kinyang’anyiro cha urais kupitia CCM, wamesema siri ya wao kukosa nafasi hiyo
ni demokrasia, haki, uwazi na utawala bora kwenye mchakato.
Kauli hizo za mawaziri wakuu zinakuja
siku moja baada ya wachambuzi kubainisha sababu 13 za wagombea wenye sifa ya
uwaziri mkuu kushindwa kupenya kwenye kinyang’anyiro hicho ndani ya CCM.
Baadhi ya sababu za wachambuzi hao ni
mawaziri wakuu hao kutetea hoja za Serikali zilizopita, kusaka mgombea
anayejiuza kwa wananchi, elimu, mtetezi wa wanyonge na haki za binadamu, asiye
na tamaa na mwajibikaji.
Warioba
Akizungumzia sababu ya yeye kukosa
nafasi hiyo ya katika chama chake, Jaji Joseph Warioba alisema anaamini
demokrasia inapewa nafasi zaidi.
Warioba alikwenda mbali na kusema CCM
inazingatia misingi ya usawa, haki na kuepuka ubaguzi, hivyo kila anayegombea
huangaliwa kwa haki sawa.
“Wakati tunachukua fomu hakuna anayeangaliwa
kwa cheo kuwa wewe ni waziri mkuu, hiyo haipo wote tuko sawa,” alisema.
Alisema ili kuhakikisha taasisi au chama
kinakuwa imara ni lazima taratibu zifuatwe, hivyo hajaona kosa kwa wao kuachwa
na kupitishwa anayehitajika au kufaa zaidi yao.
Msuya
Cleopa Msuya alisema wakati wa uchaguzi
kinachofanyika ni timu moja ambayo inakuwa na mitazamo tofauti, lakini pale
ambapo mmoja wao anachaguliwa hakuna tatizo.
Msuya alisema kinachohitajika ni
demokrasia kupewa nafasi yake na kuachana na dhana kuwa kuna upungufu au
upendeleo.
“Kwa mimi naamini kinachofanyika ni
demokrasia kupewa nafasi zaidi nadhani tuendelee kujenga nchi kwa kuwapa
ushirikiano wanaopewa nafasi ya kuongoza,” alisema.
Sumaye
Fredrick Sumaye ambaye kwa sasa ni Mjumbe
wa Kamati Kuu ya Chadema, alisema pamoja na kuwapo dhana ya demokrasia,
mchakato huo ndani ya CCM unaingiliwa na ubinafsi, hasa kwa rais anayemaliza
muda wake kutaka mtu anayehisi atamlinda.
Sumaye alisema pia ipo dhana kwa wajumbe
hujenga imani kuwa waziri mkuu amekuwa mtendaji, hivyo kumwona kama hajulikani
kwani kazi zake nyingi ni za kiutendaji zaidi.
Aidha, alisema mfumo wa upitishaji
wagombea ndani ya CCM ni sababu nyingine ambayo inawakwamisha, kutokana na Mwenyekiti
kuja na jina lake hasa akichagua mtu asiye maarufu kuliko yeye.
“Pia kuna sababu ya watu kufikiria kuwa nafasi
ya urais ni ya ulaji jambo ambalo si kweli, hivyo kusababisha vita kwenye
mchakato,” alisema.
Historia inaonesha nchini aliyefanikiwa
kutoka uwaziri mkuu na kugombea urais akashinda ni Baba wa Taifa Mwalimu Julius
Nyerere pekee, huku Warioba, Msuya, Sumaye, Edward Lowassa, Mizengo Pinda, Dk
Salim Ahmed Salim na John Malecela wakijaribu bila mafanikio.
Hali hiyo ilianza kuibua maswali kwa
wananchi wakitaka kujua siri imejificha
kwa viongozi hao kukosa kupitishwa urais.
0 comments:
Post a Comment