Jeneza tupu lazikwa kwa maiti kusahaulika


Venance Matinya, Mbeya

MAELFU ya wakazi jijini hapa, wamelazimika kusitisha shughuli zao kwa zaidi ya saa tano kushuhudia tukio la aina yake baada ya familia moja kuzika jeneza tupu na kulazimisha Jeshi la Polisi kulifukua.

Akithibitisha tukio hilo jana, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Emmanuel Likula, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 4.30 asubuhi Igoma ‘A’, kata ya Isanga.

Alisema Jeshi la Polisi la Mkoa lilipokea taarifa kuwa maiti aliyekuwa azikwe kwenye makaburi ya zamani ya Isanga alikutwa chumbani kwenye godoro na kulazimika kulifukua siku iliyofuata.

Alisema baada ya taarifa hiyo, polisi walifuatilia na kubaini kuwa juzi saa moja asubuhi Jailo Kyando (36) mwosha magari na mkewe Anna Elieza (32) wakazi wa Mtaa wa Igoma ‘A’ waliamka na kukuta mtoto wao wa kwanza Haruni Kyando (9) akiwa amefariki dunia.

Alisema taarifa za awali zilidai kuwa marehemu tangu utotoni alikuwa na matatizo ya   kifafa hali iliyosababisha aishi bila kusoma.

Kaimu Kamanda alisema kwa kifo hicho taratibu za mazishi zilifanyika na saa sita  mchana jeneza lililoletwa msibani liliwekwa sebuleni kando ya mwili wa marehemu uliokuwa umeviringishwa kwenye blanketi na kulazwa kwenye godoro.

Alisema baada ya maombi ya na Walokole wa Bonde la Baraka, vijana walibeba jeneza hadi makaburini na kuzikwa.

Aliongeza kuwa waombolezaji waliporudi nyumbani walitaharuki kuona mwili wa Haruni chumbani umelazwa eneo ulipokuwa awali.

Kutokana na hali hiyo, taarifa zilifikishwa Polisi, askari walifika na kuuchukua mwili wa marehemu na kuhifadhi kwenye mochari ya hospitali ya rufaa ya Mbeya.

Polisi walikwenda makaburini kusimamia ufukuaji kaburi kuanzia saa 4.30 asubuhi hadi saa tano asubuhi.

Baada ya kufukua Mwenyekiti wa Mtaa wa Igoma ‘A’, Fred Mwaiswelo alifunua jeneza na kukuta likiwa tupu hali iliyoashiria kuwa mwili haukuwekwa.

Polisi walibeba jeneza hilo na kwenda nalo kwenye kituo kikuu cha Polisi kwa uchunguzi zaidi kabla ya kuwakabidhi ndugu kuendelea na taratibu za mazishi kwa mara nyingine.

Hata hivyo, baadhi ya ndugu na majirani wa mtaa huo walisema tukio hilo linaweza kuwa na sura mbili; hujuma za makusudi au bahati mbaya ya kusahau mwili.  

Walisema inaweza kuwa hujuma kutokana na kawaida ya misiba kabla ya mazishi lazima ndugu kutoa heshima za mwisho, lakini msiba huo haukuwa na utaratibu huo na baadhi ya ndugu hawakuhudhuria maziko.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo