Aidan Mhando, Mwanza
WALIMU wakuu 21 wa shule za msingi
katika Halmashauri ya Ukerewe, mkoani hapa, wamevuliwa madaraka kwa tuhuma
mbalimbali zikiwamo za kuisababishia Serikali hasara ya mamilioni ya fedha kwa
kuhurusu usajili wa wanafunzi hewa.
Pia, walimu hao wamevuliwa madaraka
kutokana na matumizi mabaya ya madaraka, ikiwamo kushindwa kusimamia miradi ya
shule na kusababisha shule tano za visiwa hivyo kukosa vyoo.
Hatua hiyo ilichukuliwa na Mkurugenzi wa
Halmashauri hiyo, Frank Bahati baada kubaini kuwa walimu hao wameshindwa
kuwajibika na kukosa umakini katika kusimamia maendeleo ya shule zao, taaluma,
miradi ya shule na ukiukaji maadili.
Akizungumza na waandishi wa habari
wilayani humo hivi karibuni, Mkurugenzi huyo alisema uzembe wa walimu hao
umesababisha shule tano kufungwa kwa kukosa vyoo.
“Baada ya walimu kushindwa kutekeleza
agizo langu la kuwasilisha mpango mkakati wa kutatua changamoto katika shule zao, nimeamua kuchukua
hatua za kinidhamu,” alisema Bahati na kuongeza:
“Nawavua madaraka walimu hawa kutokana
na uzembe. Niliwaagiza kuwasilisha
mpango mkakati wa kutatua baadhi ya changamoto, lakini wameshindwa kufanya
hivyo. Shule zinakosa vyoo, ni uzembe wa hali ya juu. Miradi ya shule
inashindwa kusimamiwa ipasavyo,” alisema Bahati.
Bahati alisema walibaini kuwepo wanafunzi
hewa waliosajiliwa, matumizi mabaya ya madaraka, hali inayoonesha kwamba
wameshindwa kazi, hivyo Serikali haiwezi kuvumilia uzembe.
Serikali imekuwa ikikemea na kuchukua
hatua za kuondoa watumishi hewa jambo ambalo lilisababisha baadhi ya watumishi
wa umma kupoteza kazi kwa suala hilo
Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ina
visiwa 38, shule za msingi za Serikali 123, walimu 1,600 na wanafunzi 102,114.
0 comments:
Post a Comment