Leonce Zimbandu
Donald Trump |
SIKU chache baada ya Rais wa 45 wa
Marekani, Donald Trump ‘kuwatumbua’ mabalozi wa nchi hiyo duniani, wasomi
wameibuka na kusema hilo ni suala la kawaida, lakini kama misaada itasitishwa
Bara la Afrika litaathirika zaidi kuliko mataifa mengine.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema Marekani ni moja kati
ya nchi zinazochangia zaidi, hivyo bila shaka wanufaika wataathirika, ukiwamo Umoja
wa Mataifa (UN) wenyewe.
Alisema kama Rais Trump ataendelea na
msimamo wake wa kusitisha misaada kupitia UN, wafanyakazi wa Umoja huo watakosa
ajira kwa vile ni kati ya wanufaika namba moja.
“Lazima tufahamu uchumi wa wanufaika wa
misaada wataathirika na wengine kukosa ajira, hilo litakuwa anguko la mwaka,”
alisema.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Profesa
Mwesiga Baregu alisema hatua iliyochukuliwa na Rais Trump ni ya kawaida ili
kujipatia fursa ya kupanga safu mpya ya uongozi.
Alisema lakini kutokana na falsafa ya Rais huyo
amekuja kubana matumizi kwa nchi tegemezi, ikiwamo kutoa misaada ya fedha kwa
ajili ya bajeti na misaada mingine ya kiuchumi.
“Nchi zilizotegemea misaada kutoka Marekani zinapaswa
kujiandaa, inawezekana misaada itakayotolewa isiwe kwa kiwango
kilichotarajiwa,” alisema.
Wakili wa Kujitegemea, Alex Masaba alisema
kitendo cha kusimamishwa kwa mabalozi wa mashirika ya kimataifa kimetokana na
kusuasua kwa UN katika utendaji wake.
Alisema hiyo itakuwa njia bora kwa Rais Trump kuionesha
Dunia kuwa hafurahishwi na utendaji wa taasisi hiyo ya kimataifa na kutaka
kubadili muundo wa kiutawala.
“Kila mtawala anapoingia lazima afanye
mabadiliko ya uongozi ili kutekeleza majukumu yake kuendana na kasi ya Serikali
husika,” alisema.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania
(Jukata), Deus Kibamba alisema hakuna kitu kipya alichofanya Rais Trump kwa
vile huo ni utaratibu wa Marekani.
Alisema baada ya chama cha Damocratic kumaliza
muda wake na Republican kutangazwa mshindi, mabalozi wote walikosa sifa ya
kuendelea na nyadhifa zao.
“Unajua Trump alipotangazwa kuwa Rais, mabalozi
waliokuwa wakiwakilisha nchi hiyo walifunga virago kurudi kwao, hivyo hilo si
jambo jipya kwa Wamarekani, bali ni utamaduni wao,” alisema.
0 comments:
Post a Comment