Suleiman Msuya
Magdalena Sakaya |
HATUMTAMBUI, tunamtambua. Hivyo ndivyo
unavyoweza kusema kutokana na kauli za kutofautiana za makundi mawili ya
viongozi wa CUF, kuhusu maazimio ya Bodi ya Wadhamini wa chama hicho.
Wakizungumza na JAMBOLEO jana kwa
nyakati tofauti, viongozi hao walitofautiana kuhusu Bodi huku CUF ya Mwenyekiti
Profesa Ibrahim Lipumba ikijinadi kuwa haitambui Bodi na ya Mwenyekiti wa
Kamati ya Uongozi, Julius Mtatiro ikisema anaitambua.
Tofauti hizo zinakuja siku moja baada ya
Bodi hiyo kufanya kikao juzi na kukubaliana kufunga akaunti zote za chama hadi
mgogoro utakapomalizika kwa ilichodai ni fedha za chama kuibwa.
Naibu Katibu Mkuu Bara ambaye anatajwa
kuwa timu ya Lipumba, Magdalena Sakaya, alisema kwa mujibu wa Katiba ya CUF,
Bodi hiyo ilimaliza muda mwaka jana na kukiri kuwa haijachaguliwa nyingine
kutokana na mgogoro uliopo.
Sakaya alisema anaamini Bodi hiyo kwa
sasa haina mamlaka yoyote ya kuzuia au kufunga akaunti za chama.
“Bodi hiyo haina mamlaka kisheria na kwa
mujibu wa Katiba ya CUF, kwani muda wake ulikwisha Januari mwaka jana, hivyo
inachokifanya ni kujifurahisha, kwani sisi tunaendelea kujenga chama,” alisema.
Kuhusu utaratibu waliotumia kuchukua
fedha za ruzuku, Sakaya alisema waliomba fedha hizo kwa yeye kuandika barua kwa
Msajili ili chama kishiriki uchaguzi mdogo na shughuli zingine za kiofisi.
Naibu Katibu Mkuu huyo alisema ni
dhahiri mgogoro ndani ya CUF unawaathiri hivyo kutaka pande zinazokinzana
kuachana nao.
Aidha, Sakaya alihoji iwapo kuna upande
ambao unahoji wao kutoa fedha hizo ni kwa nini hauelezi sababu za wao kutoa Sh
milioni 86 na kuzitumia bila kuwashirikisha wao.
Mtatiro alikiri Bodi hiyo kumaliza muda wake
kikatiba lakini bado inafanya kazi kwa sababu hakuna Bodi mpya.
Alisema ukomo wa Bodi hiyo utafikiwa Baraza
Kuu la CUF litakaa na kuteua wajumbe wengine kitu ambacho hakijafanyika hadi
sasa.
“Kama anasema Bodi iliyopo si halali ni
ipi halali ambayo imeingiliwa na hii iliyopo, kimsingi wana mamlaka ya kufunga
hizo akaunti, kwani likitokea tatizo wao ndio wanashitakiwa na wakiona tatizo
wao ndio wanashitaki,” alisema.
Kuhusu Sh milioni 86 zilizotolewa chini
yake, Mtatiro alisema zilitolewa kwa kufuata utaratibu hivyo kama kuna mtu
anahoji, afuate taratibu kama wanavyofanya kuhoji Sh milioni 369 zilizotolewa
na Lipumba.
Aidha, alisema CUF haijaathirika
kutokana na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuzuia ruzuku na kubainisha
kuwa wanapata michango kwa wabunge, madiwani na wadau wengine ambao wanakipenda
chama chao.
Mwenyekiti wa Bodi, Abdallah Katao alisema
kwa sasa wako kwenye mchakato wa kufungua kesi na suala la uhalali wao liko
chini ya baraza la uongozi.
Kwa upande wake Msajili wa Vyama vya
Siasa, Jaji Francis Mutungi alisema hayuko tayari kuzungumzia mgogoro wa CUF na
kuwa wakati ukifika atafanya hivyo.
Kwa takribani miezi minne sasa, CUF
imekuwa kwenye hali ya sintofahamu ambapo kumeibuka na makundi mawili
yanayosigana; moja la Lipumba na lingine likijinadi kuwa la wafia chama.
0 comments:
Post a Comment