Shaban Njia, Kahama
Frederick Sumaye |
WAKATI Rais wa Awamu ya Tano, John
Magufuli akitekeleza masuala mbalimbali aliyowaahidi Watanzania, ikiwa ni
pamoja na kurejesha uwajibikaji na kupambana na ufisadi, Waziri Mkuu mstaafu,
Frederick Sumaye amesema hashtushwi na utendaji huo wa rais, kwani amekuwa
akitumia baadhi ya hoja na mikakati ya Chadema kuongoza nchi.
Akizungumza wakati wa kumnadi mgombea wa
udiwani katika kata ya Isagehe wilayani Kahama, Sumaye ambaye alijiunga Chadema
Agosti mwaka juzi baada ya kuachana na CCM, alisema mengi anayofanya rais ni
sera za Chadema ila chama hicho cha upinzani hakikuwa na sera ya kubana na
fedha.
Hata hivyo, Sumaye ambaye ni mjumbe wa
kamati kuu ya Chadema hakuweka wazi hoja na mikakati ya Chadema inayotekelezwa
na Rais Magufuli ambaye tangu aingie madarakani ameweka msimamo katika suala la
kubana matumizi ya Serikali, kudhibiti watumishi hewa na safari za ndani na nje
zisizo na tija na rushwa.
Katika mkutano huo ambao pia Waziri Mkuu
wa zamani Edward Lowassa alihutubia, Sumaye alisema kama wananchi, wangemchagua
Lowassa kuwa Rais, angewaletea neema ya hali ya juu kwa kuwa angekuwa na
misingi katika sera anazozitekeleza.
“Mmechagua Rais mzuri (Magufuli), lakini
anafuata sera za chama chetu (Chadema) ambazo tungezitumia kama tungekuwa
madarakani. Wananchi wa Kanda ya Ziwa mnatakiwa kumtumia Rais Magufuli ili
kufanikisha malengo yetu,” alisema huku akisisitiza kuwa hata Lowassa wananchi
wangeweza kumtumia kufanikisha malengo yao.
Huku akimnadi mgombea udiwani wa kata
hiyo, John Luzinga, Sumaye aliwataka wananchi kutofanya makosa tena ya
kuichagua CCM, ili wasije kujuta kwa maelezo kuwa watalazimika kuchagua diwani
mwingine mwaka 2020.
Alisema Chadema kinaendeshwa kwa kufuata
misingi ya demokrasia, huku akikosoa vyama kubanwa wakati nchi iriuridhia mfumo
wa vyama vingi vya siasa.
Akizungumzia sababu za kuhama CCM,
alisema kulitokana na nchi kukumbwa na hali mbaya ya uchumi sambamba na
kukosekana kwa utawala bora.
“Serikali pamoja na kubana matumizi,
hali ya uchumi imekuwa mbaya. Inatakiwa kuachia fedha ili kuwafikia wananchi
waweze kumudu ugumu wa maisha unaowakabili kwa sasa. Haiwezekani kila Serikali
isijifunze katika hili wakati hata wataalamu wanazungumza na kushauri masuala
mbalimbali,” alisema Sumaye.
Alisema kitendo cha halmashauri tatu za
wilaya ya Kahama kuongozwa na CCM, huku diwani mmoja tu ndio akiwa wa Chadema,
kitawafanya wananchi hao kukosa watu sahihi wa kuwasemea mambo yao.
Uchaguzi katika kata hiyo utafanyika
Januari 22 sambamba na kata nyingine 21 katika maeneo mbalimbali nchini.
0 comments:
Post a Comment