*Yasisitiza hakuna njaa, yakoromea wafanyabiashara
*Yakiri kukabiliwa ukame, yaonya wanaoficha
chakula
Sharifa Marira
Dk. Charles Tizeba |
WAKATI Serikali ikisema nchi haina njaa,
imeazimia kufanya tathmini ikihusisha halmashauri 55 zenye uhaba wa chakula na
kubaini kaya zenye tatizo hilo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo,
Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba, akiwa Dar es Salaam huku Waziri MKuu akiwa
Dodoma naye akiwataka wananchi kupuuza upotoshaji unaofanywa na wafanyabiashara
kuhusu hali ya chakula nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dk
Tizeba alisisitiza kuwa nchi haina njaa bali ukame katika baadhi ya maeneo na kuwataka wafanyabiashara
walioficha chakula wakitoe mara moja kabla Serikali haijatumia njia zake
kukitoa.
Dk Tizeba alisema baadhi ya watu
wanatumia ukame kupelekea ujumbe kwa jamii kuwa nchi inakabiliwa na njaa, huku
akisisitiza kuwa akiba ya chakula ipo ya kutosha.
Katika maelezo yake, Dk Tizeba alisema
wizara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Shirika la
Chakula na Kilimo Duniani (FAO) na Taasisi ya Chakula na Lishe nchini (TFNC),
wanafanya tathmini ya chakula nchini.
“Tathimini hiyo inayosimamiwa na
kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, itaiwezesha Serikali kupata taarifa za
uhakika zaidi kuhusu hali ya chakula na lishe, hasa katika maeneo yaliyoonekana
kuwa na upungufu kwenye tathmini ya awali na yaliyojitokeza baada ya tathmini,”
alisema Dk Tizeba.
Waziri Mkuu akiwa Dodoma naye aliwataka
wananchi kuepuka upotoshaji unaofanywa na wafanyabiashara kuhusu hali ya
chakula nchini, kwa lengo la kupandisha bei ya chakula.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa safari
za ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL)
mjini humo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema mwenye jukumu la kutoa taarifa
za njaa ni Serikali pekee, si vyombo vya habari wala mtu yeyote.
Ufafanuzi huo wa Serikali umekuja huku
wanasiasa na wasomi wakisema nchi inakabiliwa na njaa na Baraza la Maaskofu
Tanzania (TEC) na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), yakiwataka waumini
wao kufanya maombi, hija, mfungo kwa lengo la kukabiliana na ukame unaolikabili
Taifa.
Katika ushauri wa kada hizo mbalimbali,
juzi Mkuu wa Kanisa la Kiinjili na Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Frederick Shoo
aliitaka Serikali kufanya tathmini ya kubaini upungufu wa chakula nchini.
“Nawashangaa sana watu, kwani ukame huu
nimeuleta mimi au Kijazi (Dk Agnes- Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya
Hewa)? Wanakimbilia kulalama na kututupia maneno jambo ambalo si sawa,” alisema
Dk Tizeba.
“Ukame umekuja wenyewe, msitengeneze jambo
katika jamii na kwa bahati mbaya kauli zenu mkitoa zinaandikwa kila mahali na zinaleta
shida,” alionya Waziri.
Huku akilia na wafanyabiashara, Waziri
huyo alisema Serikali ina taarifa za wanaoficha chakula kwenye maghala
wakisubiri bei ipande na kuwataka wakitoe mara
moja.
“Waliofungia chakula wapo wengi na
tunawajua,tunaomba wakitoe na wakiuze kwa wananchi. Wasiisukume Serikali ifike hatua
ambazo si za kawaida. Hatuwezi kuwavumilia watu hao, waache chakula kiingie
sokoni, ’’ alisema Tizeba.
Alisema Serikali haitagawa chakula cha
bure kwa wananchi kwa kuwa chakula kipo cha kutosha.
Dk Tizeba ambaye pia ni Mbunge wa
Buchosa, alisema upatikanaji wa chakula nchini ni wa kuridhisha hasa vyakula
kama mchele na maharage, na kwamba upatikanaji wa mahindi si wa kuridhisha
sana.
“Pamoja na hali hii, bei za baadhi ya
vyakula zimeanza kupanda kutokana na mazao kidogo kuingia sokoni kwa wakati huu
kunakochangiwa na mwenendo usioridhisha wa unyeshaji mvua za vuli na kuchelewa
kunyesha mvua za msimu kwenye maeneo mengi nchini,” alisema.
Alisema mvua za wastani zilinyesha
Kagera, Mwanza, Geita, Kilimanjaro, Arusha, Mara, Pwani na Simiyu na mazao
yaliyopandwa katika baadhi ya maeneo hayo yaliathiriwa na ukame hususan mkoa wa
Kagera.
“Hali ya upatikanaji chakula unaridhisha
isipokuwa bei ya mahindi imepanda ikilinganishwa na mwaka jana kipindi kama
hiki. Hii inatokana na kutoingia sokoni kwa mazao mapya ya msimu wa mvua za
vuli,” alisema.
Alisema Serikali kupitia Wakala wa Taifa
wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwa mwaka huu wa fedha, imepanga kununua tani
100,000 za chakula na hadi Januari 8, ilikuwa imenunua tani 62, 087 za mahindi.
Dk Tizeba aliwataka wananchi kutumia
vizuri akiba ya chakula walichonacho na kuacha ya tamaa ya
kukiuza.
Huku akielezea kupanda na kushuka kwa bei
ya mahindi, mchele na maharage, Dk Tizeba alisema jambo hilo ni la kawaida
kutokea kwa kipindi kama hiki, kutokana na mwanzo wa msimu kukosa mazao sokoni,
hivyo kusababisha bei kupanda na mwanzo wa mavuno bei kushuka kutokana na mazao
mengi kuingia.
“Hali ya kutoridhisha ya unyeshaji mvua
za vuli umechangia wafanyabiashara wa nafaka nchini, hasa wa mahindi kuingiza
zao hilo kidogo sokoni na kuongeza kasi ya mahitaji kutoka kwa wananchi na
kusababisha bei kuzidi kupanda,” alisema huku akitaja mkoa wa Lindi kuuza kwa
bei ya juu gunia la maharage, mchele na mahindi.
Majaliwa
“Mwaka jana nchi ilikuwa na akiba ya
chakula zaidi ya tani milioni tatu hali iliyofanya baadhi ya wabunge na
wafanyabiashara kuomba kibali cha kuuza nafaka nje ya nchi.
“Serikali ilitoa kibali hicho baada ya
kujiridhisha na akiba ya kutosha ya chakula. Baada ya kibali kutoka, tani
milioni 1.5 ziliuzwa nje ya nchi,” alisema Majaliwa.
Alisema tani milioni 1.5 zilizobaki
zilihifadhiwa akiba ambapo tayari wameruhusu ziuzwe nchini ili kupunguza
kupanda kwa bei za vyakula.
“Naomba wananchi msiwe na wasiwasi juu
ya hali ya chakula nchini. Msisikilize kelele zinazopigwa na watu mbalimbali na
baadhi ya vyombo vya habari yakiwamo magazeti, kwani taarifa hizo si za kweli.
Chakula kipo cha kutosha licha ya mvua kusuasua katika baadhi ya maeneo
nchini,” alisema.
Alisema kwa kuwa mvua zimeanza kunyesha
katika maeneo mbalimbali nchini, wananchi wanatapaswa kuzitumia kulima mazao ya
muda mfupi yanayostahimili ukame.
Alisema iwapo nchi itakumbwa na uhaba wa
chakula itatoa utaratibu wa namna ya upatikanaji wa chakula kwa wananchi wake.
Kuhusu kupanda kwa bei ya vyakula kwenye
baadhi ya masoko, alisema inatokana na uhaba wa chakula nchi jirani.
0 comments:
Post a Comment