Hussein Ndubikile
WANUFAIKA wa mikopo ya elimu ya juu
wameiomba Serikali kuangalia upya sheria ya makato ya asilimia 15 ya mshahara
wanayokatwa na waajiri ili kubaki na kipato cha kutosha kujikimu kimaisha.
Awali Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa
Elimu ya Juu nchini (HESLB) ilikuwa ikiwakata asilimia 8 wanufaika walioajiriwa
lakini mwaka jana Bunge lilipitisha sheria mpya inayomtaka mwajiri amkate
mwajiriwa asilimia hiyo na wanufaika wasio kwenye ajira rasmi kutakiwa kulipa
asilimia 10 ya kipato chao.
Kauli hiyo ilitolewa juzi Dar es Salaam kwenye
msako wa ofisi kwa ofisi unaoendeshwa na Bodi hiyo na mnufaika ambaye pia ni
Ofisa Mkuu wa Ubora wa Bidhaa zinazozalishwa wa kampuni ya Tanzania Leather
Limited.
Alisema kiasi cha makato hayo
kilichoanza kutekelezwa Novemba mwaka jana hakijaangalia hali halisi ya
mishahara wanayolipwa wanufaika wenye kiwango cha Astashahada na Shahada kwenye
kampuni binafsi na mwajiriwa akikatwa na kujumlisha makato mengine, hubaki na
kiasi kidogo cha fedha kisichokidhi mahitaji muhimu.
“Hebu angalia mtu labda anapata mshahara
wa Sh 400,000 anakatwa kodi, NSSF, bima na hiyo asilimia 15 unabaki na fedha
ndogo ambazo ni vigumu kumudu gharama za maisha,” alisema.
Alisema hakatai mtu anapochukua mkopo
anakuwa na jukumu la kurejesha ila analalamikia kiwango kikubwa kilichopitishwa
na wabunge bila kuangalia hali ya maisha ya sasa ilivyo.
Meneja Urejeshaji Mikopo wa Bodi hiyo,
Deodatus Mwiliko alisema walilazimika kupendekeza kiwango hicho kutokana na
baadhi ya wanufaika kudaiwa fedha nyingi hivyo asilimia 8 isingewasaidia
kurejesha kwa haraka.
“Kuna wanufaika wanadaiwa hadi Sh
milioni 60 ukisema uwakate kwa kutumia asilimia 8 huwezi kumaliza deni inaweza
ikatokea mtu anastaafu bila kumaliza deni ilikuwa akatwe kwenye NSSF,” alisema.
Alisisitiza kuwa uamuzi huo umefanyika
kuwarahisishia wanufaika kulipa madeni yao kwa wakati.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Urejeshaji
Mikopo wa HESLB, Phidelis Joseph alisema waajiri watakaobainika kutowasilisha
majina ya wanufaika kwa wakati watatozwa faini na kuhukumiwa kifungo cha miezi
36 jela.
Meneja Rasilimali Watu wa Kampuni ya
Kamal Steels Ltd, Joseph Bryceson aliwaomba waajiri kuwasilisha taarifa ya
majina ya wanufaika kwa wakati kwa ajili ya kusaidia urejeshaji mikopo ili wengine
wenye uhitaji wanufaike.
0 comments:
Post a Comment