Salha Mohamed
DAKTARI bingwa wa magonjwa ya wanawake
na uzazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Tarimo Vecent ametaja
shinikizo la damu la juu kwamba linasababisha kifafa cha mimba, huku Mkoa wa Pwani
ukiongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi.
Ugonjwa huo unaokuwa kwa kasi katika
kipindi cha miaka mitatu iliyopita, umetajwa kusababishwa na mfumo wa maisha na
msongo wa mawazo, huku maskini wakiathirika zaidi.
Dk. Vecent alisema kifafa cha mimba
huanza wiki ya 20 ya ujauzito ambapo miongoni mwa dalili zake ni kuumwa kichwa,
presha kuwa juu, kutokuona vema, maumivu kwenye chembe.
“Wakati mwingine si lazima shinikizo
kuwa kubwa, lakini kinachosababisha ni kupungua kichwani kwa usambazaji wa hewa
ya oksijeni ndipo anapata kifafa,”alisema.
Alisema shinikizo la damu husababisha
mishipa ya damu kusinyaa na kusababisha mzunguko wa damu kuwa mdogo na kupungua
zaidi na hapo ndipo kifafa kinapotokea.
Dk. Vicent anafafanua kuwa kifafa cha
mimba hakirithiwi huku akibainisha mimba za kwanza ndiyo hupata zaidi.
“Ugonjwa huu mara nyingi huwa tunazuia
zaidi kuliko tiba kwani kila mjamzito anapopata kifafa husababisha hitilafu
kichwani hivyo matibabu huanzia kwenye kuzuia kwa kuanza kliniki mapema,” alisema.
Alisema wagonjwa wanaofikishwa
hospitalini hapo wakiwa na hali mbaya ambapo huwapa dawa aina ya Sulphatehuku
akibainisha kila mjamzito anayepata kifafa kuna kiasi cha ubongo huathirika na
kupata upungufu mwilini.
Alisema kifafa ni moja ya madhara ya
Shinikizo la damu ambapo mjamzito anaweza kupata kiharusi, kutokuona kwasababu
ya mishipa ya damu kupasuka, matatizo ya ini, matatizo ya figo.
“Shinikizo la damu husababisha viungo
vya mwili kufa kama ini,figo, kichwani huathirika yote sababu ya shinikizo la
damu kutokufuatiliwa vema tangu mwanzo,”alisema.
Alisema wanawake wengi wanaofikishwa
hospitalini hapo wanakuwa hawajitambui huku wengine wakiwa wanajitupa huku na
kule ambapo hupoteza fahamu.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha
Wagonjwa wa Kifafa cha Mimba hospitalini hapo, Alice Msondo kuzaa na wanaume
tofauti, umri mkubwa, magonjwa ya shinikizo la damu, kisukari na figo ni
miongoni mwa viashiria vya kifafa cha mimba.
“Hali duni ya maisha husababisha watu
kupata kifafa cha mimba sababu ya msongo wa mawazo, na hwapata masikini wengi
zaidi kuliko matajiri.
“Wagonjwa wengi tuliokuwa nao hapa ni
masikini mtu anakuja kujifungua hana hata kanga na ni wagonjwa wa
msamaha,”alisema.
Alisema katika hospitali hiyo hupata
wagonjwa 80 hadi 120 kwa mwezi huku idadi hiyo ikionekana kuongezeka katika
miaka mitatu.
“Tatizo linakuwa hasa miaka mitatu hii,
kutokana na hali ya maisha msongo wa mawazo na hata hali ya hewa kama ambavyo
Pwani huathirika zaidi,”alisema.
Alisema ugonjwa huo hauchaugui umri
kwani hupata wenye umri wa miaka 16, mimba za kwanza na hata wenye umri mkubwa.
Alisema wanawake wengi wanaopata ugonjwa
huo hupoteza watoto au kupata mtoto njiti ambapo hospitali huakikisha anajifungua
ndani ya saa 8 ili kuokoa maisha ya mama.
Aliitaka jamii kutambua muhimu wa kuwahi
kliniki, kutambua muda wa kubeba mimba ili kuepuka msongo wa mawazo na kupata
madhara kwani ni ugonjwa wa pili kusababisha vifo vya mama na mtoto nchini.
0 comments:
Post a Comment