Mwandishi Wetu
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa |
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakurugenzi
wa halmashauri na manispaa nchini kutowapa fedha taslimu madiwani kufanyia kazi
za maendeleo.
Badala yake ametaka waandae mfumo maalumu
wa kutoa fedha hizo kama zinavyotolewa za Mfuko wa Jimbo ambazo ni maalumu kwa
wabunge lakini zinatumika kwa maendeleo jimboni.
Alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na
viongozi na watendaji wa Mkoa wa Ruvuma baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo
kwenye Ikulu ndogo ya Songea.
“Nimepata taarifa kuwa fedha za
maendeleo kwa madiwani zinakabidhiwa mikononi. Hapana. Msiwape fedha mikononi,
zifuate mfumo wa utoaji fedha wa Serikali. Kama mlikuwa na matumizi ya aina
hiyo, mwisho wake ni jana (juzi),” alisisitiza.
“Fedha za Mfuko wa Jimbo ni za Mbunge,
lakini hapewi mkononi bali zinapelekwa kwenye Halmashauri naye anahusika kwenye
kikao cha uamuzi. Anakubaliana na madiwani wenzake ni miradi ipi ipewe fedha,
ambayo mara nyingi inakuwa imekwishaidhinishwa na vikao husika,” aliongeza.
Alisema makusanyo ya fedha yanayofanywa
na Halmashauri hayana budi kuangaliwa pia na jinsi fedha hizo zinavyotumiwa.
“Lazima tukishakusanya tuangalie tumepata kiasi gani, si kukaa na kuamua kutoa
Sh 500,000 kwa kila diwani. Suala la matumizi ni muhimu sana, ni lazima fedha
hizo ziende kwenye miradi ya maendeleo,” alisisitiza.
Alisema kuna baadhi ya watu hugawana
fedha kwa kigezo cha maendeleo, lakini wanaishia kutumia fedha hizo kwa kigezo
cha kujengeana uwezo. “Hii si sahihi na jana nilipiga marufuku posho za aina
hii pamoja na za vitafunwa, kwa sababu zinaishia kwa wakubwa wachache na
waliozikusanya hawapati chochote,” aliongeza.
Akizungumzia ukusanyaji wa mapato kwenye
Halmashauri, Waziri Mkuu aliwataka waangalie baadhi ya kampuni ambazo zinajitokeza
kutoa vifaa vya kukusanya ushuru.
0 comments:
Post a Comment