Charles James
Ukarabati Reli ya Kati |
SHIRIKA la Reli Tanzania (TRL) limeanza
ukarabati wa Reli ya Kati kuanzia stesheni ya Dar es Salaam hadi kituo cha Pugu
utakaochukua wiki 10 kwa Sh bilioni 12.5.
Akizungumza jana, Mhandisi Mkuu wa Shirika
hilo, Nelson Ntejo alisema ukarabati huo ni wa kawaida kutokana na reli kukaa
kwa muda mrefu bila kubadilishwa, ili kuboreshwa kutokana na iliyopo kushindwa
kubeba kiasi kikubwa cha mizigo.
Ntejo alisema ukarabati huo ulianza
Januari 2, na hauna uhusiano wowote na mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ambao
uliahidiwa na Rais John Magufuli kwenye kampeni zake.
“Haya ni maboresho ya kawaida tu ambayo
TRL imeamua kufanya ili kuboresha reli zake ili treni zibebe mizigo yenye ujazo
mkubwa zaidi lakini pia itaongeza kasi ya treni kutoka spidi 30 hadi 50,”
alisema.
“Lengo ni treni za abiria zinazotoka
Pugu kwenda Stesheni kuwa na kasi na ubora zaidi ili kushindana kibiashara na
daladala ambapo tunaamini tutafanikiwa na kuongeza mapato ya Shirika na Taifa
kwa jumla,” alisema Ntejo.
Akitaja mchanganuo wa gharama za ujenzi
huo, alisema Sh bilioni 12 zitatumika kununua mahitaji ya vifaa vya matengenezo
huku Sh milioni 500 zikitumika kulipa wafanyakazi kwenye mradi huo ambao wako
100.
“Kazi hii ni endelevu si kwamba itaishia
hapa tu na awali tulianza Msata hadi Mpiji ambapo tulitengeneza kilometa 12
hivyo baada ya hapa tutaendelea na maeneo mengine ili kuboresha na kurahisisha
usafiri nchini, huku pia ukiwa salama kwa watumiaji.
0 comments:
Post a Comment