Mariam Cyprian, Tanga
WATU 12 waliokuwa wakisafiri na mashua
iliyokuwa ikitoka Tanga kwenda Pemba wamekufa maji na miili yao kuopolewa baada
ya chombo hicho kukumbwa na dhoruba iliyotokana na upepo mkali wa Kaskazi.
Abiria 34 waliokolewa na wavuvi
waliokuwa wakivua kwenye bahari ya Hindi eneo la Jambe jirani na pwani ya mkoa
wa Tanga.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana na
kuthibishiwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba, mashua
hiyo iliyokuwa ikiendeshwa na nahodha Badru Said ilipigwa na dhoruba saa mbili
usiku wa kuamkia jana.
Abiria walionusurika walisema chombo
hicho kiling'oa nanga kwenye bandari ya Sahare jijini hapa juzi saa moja usiku kwenda
Wete, Pemba ikiwa na abiria 52 na shehena ya mizigo ikiwamo mifuko ya mchele, pumba,
viazi, maharage na masanduku ya bia.
Walisema baada ya kufika eneo la Jambe
mashua hiyo ilipigwa na dhoruba kwa nyuma na kupoteza mwelekeo na kwa kuwa
kulikuwa na upepo mkali, abiria walizama baharini.
Mkubwa Yussuph Hassan (55) alisema
kuzama kwa mashua hiyo, kulitokana na kutoboka kwa chini na maji kuingia kwa
kasi na ndani ya dakika 15 yalijaa na kusababisha kila kilichokuwamo kulowa.
"Kitendo hicho cha kupigwa na
dhoruba kilikuwa ni cha muda na chombo kujaa maji kilikuwa ni cha muda mfupi
sana hivyo hatukuwapigia simu jamaa zetu wa Pemba na Tanga kwa sababu simu
zilijaa maji na kushindwa kufanya kazi," alisema Mkubwa mzaliwa wa Pemba
na mkazi wa mtaa wa Nguvumali jijini hapa.
Mussa Isah Mohamed (37) wa Kengeja,
Pemba aliyekuwa na mtoto wa kaka yake, alisema yeye alinusurika baada ya
kuogelea hadi kufikia chombo cha wavuvi.
"Nasikitika mtoto wa kaka
niliyekuwa nakwenda naye Pemba amekufa, ilifika mahali nilishindwa kumwokoa
nikawa sina jinsi zaidi ya kumuaga na kumwambia ‘tangulia ndugu yangu hakuna
namna’," alisema Mussa huku akitokwa machozi.
Aidha wavuvi waliofanya uokoaji walisema
baada ya kubaini kuwa mashua hiyo imezama, walipiga mbizi na kuibua miili ya
waliokufa na wengine waliokuwa hai.
"Tunashukuru Mungu alitupa nguvu ya
kupiga mbizi kwenye maji marefu ya Jambe, tuliokoa abiria 34 na miili ya tuliokuta
wameshakufa maji," alisema Mbwana Hamis Mbwana.
Kamanda Wakulyamba alisema abira 12 akiwamo
nahodha wa mashua hiyo, Badru walikufa maji huku wengine 34 wakiokolewa na
kufikishwa hospitali ya Bombo kwa matibabu.
Alisema mashua hiyo iliyotoka jijini hapa
kutoka bandari bubu ya Sahare, ilikuwa imebeba magunia 30 ya pumba, mchele
magunia 10, maharage magunia 15 na masanduku ya bia.
Kamanda alisema majina ya waliokufa na
majeruhi atayataja baada ya ndugu zao kuwatambua.
Ofisa wa Mamkala ya Udhibiti wa Usafiri
wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) Mkoa wa Tanga, Dk Walukani Luhamba alisema
ajali hiyo ni matokeo ya manahodha kupuuza maelekezo ambayo yamekuwa yakitolewa,
kuhusu kufuata sheria na taratibu za usafiri majini.
0 comments:
Post a Comment