MGOGORO ndani ya CUF umeendelea kuibua
mapya baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi, Julius Mtatiro kueleza jinsi
Profesa Ibrahim Lipumba alivyochukua fedha za ruzuku zaidi ya Sh milioni 300 Hazina
bila utaratibu.
Amesema Bodi ya Wadhamini ya Chama hicho
inakutana na kamati tendaji kutafakari ‘shambulio’ hilo kubwa la chama na
kutekeleza hatua za kiutawala na kisheria za kuchukua na kwamba wanasheria wako
tayari kupokea maelekezo kwa ajili ya kulinda chama.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mtatiro
alisema suala hilo ni la kushangaza kwa kuwa Oktoba 10 mwaka jana, Msajili wa
Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi aliandika barua ya kusitisha utoaji
ruzuku kwa chama hicho, akihofia migogoro iliyokuwa ikiendelea na kueleza kuwa
hadi hali itakapokuwa shwari kiutendaji kuwezesha viongozi husika kusimamia
matumizi ya fedha hizo ipasavyo ndipo ruzuku hiyo itatoka.
Aidha, alisema tangu Msajili aandike
barua hiyo ya kusitisha ruzuku, chama kinaidai Hazina Sh milioni 635, kwa kuwa
barua za usitishaji zipo na kwa kuwa CUF haitambui utaratibu mwingine wa kugawa
ruzuku.
Alisema chama hicho kimeibiwa fedha za
ruzuku Sh milioni 369 na zilitoroshwa kutoka Hazina ya Serikali Kuu Januari 5 na
kuingizwa kwenye akaunti ya NMB tawi la Temeke yenye jina la The Civic United
Front ikiwa na akaunti namba 2072300456.
"Bodi ya Wadhamini wa CUF ambayo
ndiye msimamizi wa jumla wa masuala ya akaunti za fedha na mali za chama,
haitambui akaunti hiyo na haikuwahi kuiidhinisha ipokee ruzuku ya CUF kutoka Serikali
Kuu, Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad ambaye ndiye mwajibikaji mkuu wa
masuala ya kifedha na mali za chama, haitambui akaunti hiyo," alisema.
Aliongeza kuwa Maalim hajawahi kumwandikia
Msajili au kumpa akaunti hiyo, aweke fedha za ruzuku ya CUF na kwamba vikao vya
kitaifa vya chama kwa maana ya Kamati Tendaji ya Taifa na Baraza Kuu la Uongozi
hawakuwahi kupitisha uamuzi huo wa fedha kuwekwa kwenye akaunti hiyo ya wilaya
iliyoko NMB tawi la Temeke.
"Baada ya kugundua utoroshwaji huo
wa fedha za ruzuku ya CUF ambazo ni za umma zenye masharti na taratibu zake
katika kutolewa, tumejiridhisha kuwa akaunti ambayo Hazina walishiriki kuitumia
kutorosha fedha za umma na mali za CUF, ni akaunti ya chama ambayo hutumiwa na
wilaya ya Temeke kupokea mgao wa ruzuku kutoka chama Taifa," alisema.
Alisema CUF ina akaunti kila wilaya ya
kichama, huku akitolea mfano Kinondoni yenye benki ambayo huitumia kupokea
fedha zilizoidhinishwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa ya Chama kwa mujibu wa Katiba,
wilaya ya Ilala pia ina akaunti ya aina hiyo, Mtwara na mikoa mingine.
Alisema baada ya watu wanaomsaidia
Profesa Lipumba ambaye alimwita 'Bwana yule' kuona kwamba Bodi ya Chama imezuia
njama za ufunguaji akaunti mpya ya CUF, walitumia mbinu mpya ya aina hiyo hiyo
kwa njia tofauti na siku mbili kabla ya utoroshwaji wa fedha hizo, waliondoa
baadhi ya viongozi Temeke kwenye kusaini akaunti hiyo.
Alieleza kuwa uondoaji viongozi hao
ulikwenda sambamba na kugeuza baadhi ya wateule wa Lipumba wanaofanya kazi za
kuhujumu chama kutokea Buguruni, kuwa watia saini wa akaunti ya wilaya ambao ni
Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya na Thomas Malima.
Alisema siku moja baada ya NMB na wala
njama kukamilisha mchakato wa kubadilisha watia saini wa akaunti ya CUF inayomilikiwa
na wilaya ya Temeke, Hazina iliweka fedha hizo bila kuchelewa na siku hiyo hiyo
watia saini wapya wa akaunti ya NMB Temeke, waliulizia kiasi cha fedha
kilichomo kwenye akaunt hiyo na walifanya hivyo kwenye tawi la Barabara ya
Mandela.
Alifafanua kuwa siku iliyofuata Januari
6 watia saini hao wakiongozwa na Malima walikwenda NMB Temeke na kutoa Sh milioni
69 kisha wakahamisha Sh milioni 300 kutoka akaynti namba 41401600207 kwenda
kwenye akaunti ya mtu binafsi aliyejulikana kwa jina la Mhina Omary ambaye ni
Diwani wa CUF wa Wilaya ya Handeni.
Zahamishwa
Akizungumzia namna Omary alivyohamisha
fedha alifafanua kuwa Januari 6 aliondoa Sh milioni 100 kutoka NMB tawi la
Magomeni, akaongeza Sh milioni 50 kisha akaelekea tawi la Kariakoo na kutoa Sh
milioni 100 na kuongeza akaongeza milioni 49.5.
Alisema wakati Omary anazunguka kwenye
matawi hayo kutoa fedha alikuwa na ulinzi wa polisi waliovalia kiraia kwenye
magari ya CUF akifuatana na Malima chini ya usimamizi wa watu wawili ambao ni
Sakaya na Kambaya.
Alisema baada ya fedha hizo kuhamishwa
akaunti yake ilibaki na Sh 207 kama zawadi kwa kuwa wakati anaweka Sh milioni
300 hakukuwa na hata senti tano na kwamba fedha zilizotoroshwa na kupelekwa
kusikojulikana ilikuwa ni kabla chama kupata taarifa kuhusu wizi huo.
JAMBO LEO ilimtafuta Profesa Lipumba ili
kutolea ufafanuzi suala hilo, simu yake iliita bila majibu lakini Kambaya
alisema ni kweli fedha hizo waliomba Hazina kwa kuwa Lipumba anatambulika kama
Mwenyekiti wa Chama.
"Nashangaa sana mnashindwa kuelewa
nini, fedha tumeomba na tumepewa kwa ajili ya shughuli za kichama si vinginevyo,
kwa kuwa Lipumba ni Mwenyekiti wa Chama," alisema.
0 comments:
Post a Comment