Sharifa Marira, Rufiji
MBUNGE wa Rufiji, Mohammed Mchengerwa ameeleza
kusikitishwa kwake na kitendo cha Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads) mkoa
wa Pwani, kutoa kibali kwa taasisi ya walemavu ili kuvunja daraja lililojengwa
kuelekea lilikopita bomba la gesi wilayani humo na kukiita ni uhujumu
uchumi.
Daraja hilo lililojengwa kwenye kijiji cha Umwe Kusini
kwa msaada wa Serikali ya China kwa zaidi ya Sh bilioni moja, lilivunjwa
Novemba 28 mwaka jana na kusababisha wananchi kushindwa kuvuka kwenda eneo la
bomba la gesi.
Akiwa katika eneo hilo, Mchengerwa alikabidhiwa barua ya
Tanroads Mkoa kama kibali cha kuchukua chuma chakavu na makalvati mabovu.
Akisoma barua hiyo mbele ya wananchi wa eneo hilo,
Mchengerwa alisema barua hiyo iliyosainiwa na aliyekuwa Meneja wa
Tanroads wa Mkoa, Tumaini Sarakikya ilichangia kubomolewa kwa daraja hilo
baada ya Meneja huyo kuagiza kutafutwa kwa vyuma chakavu katika barabara za
wakala huo.
"Barua hiyo ya Agosti 3 mwaka jana, ilielekeza
kutafutwa vyuma chakavu katika barabara zilizo chini ya Wakala huo lakini si za
Halmashauri kama ilivyofanyika kwenye eneo hilo," alisema Mchengerwa.
Alisema aina hiyo ya uharibifu wa miundombinu haukubaliki
na kufananisha tukio hilo na uhujumu uchumi ambao hauvumiliki.
"Hii ni kesi ya uhujumu uchumi, kwa sababu ni
uharibifu wa miundombinu, thamani ya uharibifu wa mali hii inafaa watu hawa
kupelekwa katika Mahakama ya Mafisadi… wamekuja kuvunja daraja ambalo tulipata
msaada wa zaidi ya Sh bilioni moja, kwa nini tunarudishwa nyuma? Kwa sasa
watu wanaokwenda lilipo bomba la gesi hawawezi kwenda, njia hakuna," alisema
Mchengerwa.
Hata hivyo, Mbunge huyo alieleza kuwa alizungumza na
Kaimu Meneja wa Tanroads wa Mkoa, Yudas Msangi ambaye alieleza kutofahamu
jambo hilo na kutihusika na kibali hicho.
Msangi aliahidi kufuatilia jambo hilo akieleza kuwa
huenda kuna watendaji wa ofisi yake wasio waaminifu wanaoshirikiana na watu
wengine kufanya hujuma hizo.
Hata hivyo, pamoja na Msangi kukataa kujua jambo hilo,
juzi maofisa waliojitambulisha kutoka Tanroads walifika eneo hilo wakiomba
ushirikiano wa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM wa Wilaya ya Rufiji, Mussa
Mng'eresa, kuangalia namna uharibifu ulivyotokea.
Akizungumzia suala hilo, Mng'eresa alisema: "Hawa
watu waliojitambulisha wanatoka Tanroads ni bandia, lakini nashangaa wanatumia
gari la Wakala huo wakati Kaimu Meneja anadai hana taarifa, hatuelewi hawa watu
wanatuchanganya."
0 comments:
Post a Comment