Dotto Mwaibale
WANANCHI wa
Mbagala Sabasaba wamemuua kwa mawe na kumchoma moto kijana aliyetuhumiwa
kujihusisha na uhalifu wa kundi maarufu jijini Dar es Salaam la ‘panya road’.
Mbali na kijana huyo ambaye hakupatikana jina, wenzake wawili kati ya zaidi ya
15 waliokuwa pamoja walijeruhiwa mpaka kupoteza fahamu.
Mauaji hayo
yalifanyika jana saa 11 jioni katika eneo hilo baada ya vijana hao kukurupushwa
kutokana na madai ya kufanya uhalifu maeneo ya sabasaba Magengeni na Mbagala
Zakhem.
Polisi
walifika eneo la tukio na kulazimika kutumia risasi za moto kutawanya wananchi,
kabla ya kuchukua mwili wa kijana huyo.
Akizungumza
na mwandishi wa Jambo Leo, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye
alijitambulisha kwa jina moja la Khalfan, alidai kuwa usalama wa wananchi upo
mashakani kutokana na vitendo vya kundi hilo la ‘panya road’.
“Hawa
‘panya road’ walikuwa zaidi ya 15 wakitokea Mbagala Zakhem ambako walikuwa
wakikimbizwa na wananchi baada ya kufanya uhalifu na walipofika hapa Sabasaba,
walizingirwa na wananchi ambapo watatu kati yao walishambuliwa na mmoja
kapoteza maisha baada ya kuchomwa moto,” alidai.
Alidai
vijana wawili kati yao walijeruhiwa vibaya na kupoteza fahamu lakini wenzao wengine
walifanikiwa kukimbia kwenda maeneo ya Yombo Dovya, huku wakiahidi kurudi
kulipiza kisasi cha kuuawa kwa mwenzao.
Mkazi
mwingine wa Mbagala kwa Mangaya, Seif Mwarami alidai vijana hao wataendelea
kuuawa na wananchi kwa kuwa kila wanapokwenda kutoa taarifa Polisi, hawachukuliwi
hatua yoyote badala yake wanaachiwa na kurudi mitaani kuendeleza uhalifu.
Alidai kuwa
vijana hao wana umri mdogo ndio maana hawapelekwi mahakamani kutokana na
kulindwa na sheria za watoto, jambo linalowatia hasira wananchi na kuamua
kujichukulia hatua mkononi.
Kwa mujibu
wa madai ya Mwarami, vijana hao wamekuwa wakitokea maeneo ya Kitunda, Moshi Baa
na Yombo kwenda kufanya uhalifu Mbagala.
Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, Kamishna Msaidizi (ACP), Gilles Muroto
alipopigiwa simu jana jioni alisemaalikuwa kwenye mkutano hivyo apigiwe baadae.
0 comments:
Post a Comment