·
* Mangula
aonya wamebainika, watakiona
Sharifa Marira na Leonce Zimbandu
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM, Philipo Mangula, ameanza kupokea majalada
ya wanaCCM walioanza kujipitisha kutoa rushwa kwa ajili ya uchaguzi wa ndani wa
chama hicho, unaotarajiwa kufanyika mwakani.
Amesema ana taarifa kwamba baadhi ya wana CCM wameanza kutumia
mbinu chafu za fedha kutaka nafasi mbalimbali, lakini ‘imekula kwao’ kwa kuwa
hawatapenya kwani atawashughulikia.
Mangula alitoa kauli hiyo jana Dar es Salaam, wakati akitoa mada ya
maadili ya viongozi kwenye kongamano la maadhimisho ya kumbukizi ya Mwalimu
Julius Nyerere na kueleza kukerwa na tabia ya wafanyabishara wenye fedha kutaka
kuteka kila mahali.
Alisema ndani ya CCM yeye ni maarufu kwa jina la ‘Mzee wa Mafaili’,
hivyo ataendelea kupitia majalada hayo ili kuhakikisha maadili yanazingatiwa na
kuenzi misingi ya Azimio la Arusha, kwani hakuna atakayepenya kwa rushwa.
“Zipo taarifa kuwa wapo baadhi wameanza kujipitisha na kutoa rushwa
kwa ajili ya uchaguzi wa mwakani, nawahakikishia kwangu watu hao hawawezi
kupita, nitamfuatilia kila mmoja atakayejihusisha na rushwa ili asipate nafasi hiyo,”
alisema.
Kutenganisha
Alisema ili kudhibiti mianya hiyo, atahakikisha sheria inatungwa ya
kutenganisha kati ya wafanyabiashara na uongozi, kwa vile wafanyabiashara wanatafuta
nafasi ya uongozi, ili kuendeleza biashara zao.
Mangula alisema ni aibu kwa mpigakura kuhongwa kiasi kidogo cha
fedha na kupoteza haki ya msingi ya kuchagua kiongozi mwenye sifa kwa ajili ya
maendeleo. Alisema iwapo tabia ya kununua uongozi itaendelea, baadaye vijana
wanaohitimu masomo watakosa nafasi za kugombea kutokana na kukosa fedha za
kuhonga.
Watanzania wanapaswa kufahamu hatua zinazochukuliwa na Rais John
Magufuli, kuwatumbua watumishi wazembe, imetokana na kauli ya vikao halali vya
CCM ili atekeleze hayo.
“Huo ni mpango mkakati wa chama, kwa lengo la kuondokana na rushwa,
vinginevyo misingi na maadili ya uongozi vitapotea,” alisema.
Spika mstaafu na Mwenyekiti wa Kongamano hilo, Anne Makinda
aliwataka vongozi wa vyama vya siasa kupeleka vijana wao kwenye Chuo cha
Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere (MNMA) kujifunza maadili ya uongozi ili kuepuka
rushwa.
Alisema kongamano hilo lilizingatia mada kuu tatu; Azimio la
Arusha, Miiko ya Uongozi na Maadili ya Viongozi, ambayo yanapaswa kutumiwa na
kila kiongozi kujitathmini.
Mmoja wa watoa mada, Katibu Mkuu wa CCM mstaafu, Wilson Mukama
alisema viongozi wengi wa siasa wapo kwa ajili ya maslahi binafsi ya kupata
utajiri, zikiwamo nyumba, magari na fedha. Alisema hali hiyo inawafanya watumie
gharama yoyote kupata nafasi ya uongozi huku akijua fedha hizo zitarudi na
kutengeneza maisha mapya.
“Wapo viongozi kwa ajili ya maslahi yao na si maslahi ya jamii,
huko ni kutoka nje ya maadili,” alisema.
“Viongozi wengi wanashughulika na matatizo yao binafsi ndio maana
hata wabunge walilalamika walipopewa Sh milioni 95 za kununulia magari
walipoingia madarakani wakadai ni ndogo, ushabiki wao ni magari, nyumba na fedha
lakini si waliowachagua,’’ alisema Mukama.
Butiku
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku alisema
kiongozi wa nchi hapaswi kuongoza kama tembo badala yake anapaswa kuheshimu wananchi
akitambua kuwa binadamu wote ni sawa jambo ambalo Mwalimu Nyerere
alilisisitiza.
‘’Ukitaka kuwa kiongozi wa nchi hii unapaswa utambue na uwe na
imani kwamba watu wote ni sawa, usiwe Rais tembo unapaswa kujua kuwa watu
unaoongoza unatokana nao na uwaongoze kwa heshima,’’ alisema na kuongeza:
’’Ukitaka kuwa Spika unapaswa ujue unaongoza wabunge
wanaotuwakilisha sisi, hivyo uongoze ukijua kwamba wabunge wanawakilisha watu
wengi, chagua unataka kuwa kiongozi wa watu unaotumwa na watu au unataka kuwa
kiongozi wa kutafuta utajiri na kuongoza matajiri,’’ alisema.
Alisema wanasiasa wengi hawasikilizi wanaowachagua, ndiyo maana
wanakuwa maadui wa wananchi kutokana na kwenda kinyume na matakwa yao.
“Viongozi wengi nchi hii ni wababaishaji, mnakuwa maadui wa
wananchi kutokana na kwenda kinyume na wanavyotaka, mko nje ya mstari wao,
acheni kubabaisha, Nyerere alikuwa binadamuna aliamini kwa binadamu, Imani yake
ilikuwa kwa watu wote na ndicho kiini cha mambo yote, Imani katika watu, watu
wote ni watu hakuna mtu mbuzi, kuku wala paka,’’ alisema Butiku.
Butiku alisema hata mwaka 1985 wakati Mwalimu Nyerere anaaga bungeni,
alisema kazi muhimu kuliko zote kwake na kwa wananchi wote ni kujenga Taifa
lenye umoja kwa msingi wa heshima na usawa kwa binadamu.
Kondo
Kanali mstaafu,Dk Harun Kondo alisema Azimio la Arusha ndilo
linalotambulisha Taifa hivyo ni vigumu kuliua na atakayejaribu atakufa yeye,
kutokana na kuwa na misingi ya kisayansi, likizungumzia matatizo halisi ya
wananchi.
“Suala la rushwa nchini limekuwa kama dini, imani za watu ni rushwa
pekee, tumekuwa kama kiwiliwili kinachotembea, tumeondoka katika misingi ya
Azimio na siasa za Ujamaa na Kujitegemea tumekwenda kupotelea tunakokujua wenyewe,’’
alisema Dk Kondo.
0 comments:
Post a Comment