Fidelis Butahe
SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya
Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba kuwasimamisha kazi
wakurugenzi sita wa idara za chama hicho, wasomi wamemtaka kutumia busara ili
kunusuru mvutano na vurugu zinazoweza kukikumba chama hicho.
Wamesema licha ya kuwa mtaalamu huyo wa uchumi kuwa anasimamia
Katiba ya chama hicho kurejea katika nafasi yake, lakini ni jambo la kushangaza
kutaka kurejea katika wadhifa huo takribani mwaka mmoja baada ya kujiuzulu,
huku wakihoji alisahau nini.
Juzi Lipumba alitangaza kuwasimamisha kazi wakurugenzi hao kutokana
na changamoto zinazokikabili chama hicho, jambo lililopingwa na Kaimu
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Ismail Jussa Ladhu
aliyeeleza kwamba Lipumba hana uwezo huo na kusisitiza wakurugenzi hao
wanaendelea na majukumu yao kama kawaida.
Katika maelezo yake, Profesa Lipumba alisema atateua watakaokaimu nafasi
hizo hadi watakapothibitishwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha,
Profesa Gaudence alisema: “Lipumba atumie busara tu. Hivi hii hali iliyopo CUF
anaionaje? Alijiuzulu mwenyewe sasa anarudi vipi? Alipaswa ajipime mwenyewe;
je, anakubalika? Maana mkutano mkuu wajumbe zaidi ya 400 walipinga kurejea
kwake katika uongozi.”
“Kwa kilichotokea katika mkutano huo alipaswa tu kukaa kando. Hata
vyama vinavyounda Ukawa havipo pamoja naye sijui atafanyaje kazi. Atasimamia wapi,”
alisema msomi huyo Wakili na mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk James
Jesse alisema:
“Kujiuzulu na kukaa mwaka mzima kasha kutangaza kurejea ni jambo
ambalo halikubali kisheria na kikatiba.” Alisema kwa uamuzi huo wa kujiuzulu,
kuendelea kumtambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti wa CUF licha ya kuwa
anatumia Katiba ya chama hicho kueleza uhalali wake si sahihi.
Hata hivyo, akizungumzia uamuzi wake, Lipumba alisema: “Katiba
inasema (mwenyekiti) anashauriana na makamu mwenyekiti katika kuteua, ila katika
kubadilisha mimi ndio nabadilisha na kupeleka majina katika Baraza Kuu la
Uongozi Taifa kuthibitisha.”
Alipoulizwa kama hilo litawezekana kutokana na baraza hilo kupiga
kura ya kumvua uanachama alisema: “Ni mpaka wakati ukifika…, nitapeleka majina
katika Baraza Kuu ili kuthibitishwa. Kuna kazi ngumu, ila nina nia ya umoja na
kufanya kazi ya pamoja kwa ajili ya kujenga chama pande zote mbili za
muungano.”
0 comments:
Post a Comment