* Yeye ampa masharti Maalim kuingia ofisini
* Adai akaunti ya chama haina hata senti moja
Sharifa Marira na Eme resiana Athanas
WAKATI Mwenyekiti wa CUF aliyefutiwa uanachama, Profesa Ibrahim
Lipumba akitangaza masharti kwa Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad ya kuingia
kwenye ofisi za chama hicho Buguruni, Dar es Salaam Chadema imetangaza
kutoshirikiana naye.
Akizungumza kwenye makao makuu ya Chadema jana, Mwenyekiti wa chama
hicho, Freeman Mbowe aliwataka viongozi wa chama chake, kutotoa ushirikiano kwa
Profesa Lipumba, badala yake wampuuze na wamwone kuwa msaliti wa harakati za kudai
haki.
Wakati akisema hayo, Profesa Lipumba akiwa katika Ofisi Kuu za CUF,
alitoa masharti kwa Seif kama anataka kufika ofisini hapo, kuwa lazima akiri
kumtambua na kumkubali kuwa Mwenyekiti halali wa chama hicho.
Chadema
Mbowe katika mkutano wake na waandishi wa habari, alisema Lipumba,
Msajili wa Vyama vya Siasa na taasisi ya utafiti ya Twaweza, ni mawakala wa
Serikali wa kuzia harakati za kupigania demokrasia nchini.
Alisema harakati za kuzuia wapinzani kupigania haki, hazifanywi
moja kwa moja na Serikali, bali na wakala wao ambao wanakuja kwa sampuli
mbalimbali.
“Kamati Maalumu ya Kamati Kuu inatambua mgogoro ndani ya CUF, hivyo
chama chetu hakimtambui Profesa Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF wala Mwenyekiti
Mwenza wa Ukawa.
“Kamati inalaani uamuzi wa Jaji Francis Mutungi wa kuivuruga CUF
kwa kujaribu kumrudisha madarakani Lipumba ambaye alijiuzulu katika mazingira
yanayoashiria kununuliwa na CCM, kwa lengo la kusaliti Ukawa kwenye uchaguzi
mkuu wa mwaka jana,” alituhumu.
Kuhusu Jaji Mutungi, Mbowe alimtangaza kama adui wa demokrasia na
vyama vingi na kudai kuwa pamoja na kuwa Jaji, hana weledi wa kusimamia vyama vya
siasa.
Alitumia nafasi hiyo kubainisha kuwa chama hicho hakina sababu hata
moja ya kumheshimu mtu kama Jaji Mutungi ambaye alisema anaonekana kutumika na CCM.
“Mtu ambaye tunamwona msomi, ambaye hapewi mamlaka yoyote ya
kisheria ya kuamua ndani ya vyama vya siasa, badala ya kusaidia vyama kumaliza
migogoro, amekuwa akichangia migogoro.
“Anaona vyama vinaminywa na Serikali anakaa kimya, lakini kila
akizungumza anavikandamiza zaidi, huyu mtu ni adui mkubwa sana,” alisema.
Alimhakikishia Jaji Mutungi kuwa mbinu zake za kudhoofisha vyama
vya upinzani hazitafanikiwa, kwani hakuwa Msajili wa kwanza, na kwamba matendo hayo
hayatafifisha vyama hivyo.
Kuhusu Twaweza, alidai kuwa imekuwa ikilipwa na Serikali itangaze
mambo mbalimbali siku moja kabla ya Ukuta kwa kutoa takwimu alizoziita za
kipumbavu na kwamba wamekubali kujitwisha uendawazimu.
“Hawa ni mawakala wa Serikali na wanajulikana. Ni Mtanzania
mwendawazimu pekee ambaye utamwambia kwamba hali ya nchi, Serikali inakubalika
kwa asilimia 96, lazima uwe mwendawazimu na utafiti huo hauwezi kulisaidia
Taifa,” alisema.
Masharti CUF
Wakati Chadema ikitoa kauli hiyo, hali ya kisiasa ndani ya CUF
ilizidi kuwa mbaya kutokana na pande mbili zinazosigana kutunishiana misuli.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari waliofika Ofisi Kuu zaCUF
jana, Profesa Lipumba alisema alipata taarifa kwamba Maalim Seif angefika
ofisini hapo juzi, hivyo alimsubiri ampangie kazi.
Alisema kama Seif angefika, kabla ya kufanya kazi na Mwenyekiti
jambo la kwanza ingekuwa ni kumtambua kwa nafasi hiyo ambayo alivuliwa na kikao
kisicho halali.
“Ni lazima akija hapa afanye kazi na Mwenyekiti na walinzi wetu
wanamfahamu, wasingemfanya chochote kwa kuwa ni kiongozi wao pia,” alisema na kuongeza:
‘’Huwezi kuja ofisi za chama, halafu ukasema humtambui Mwenyekiti,
analijua hilo kwamba akija hapa ni lazima afanye hivyo, kwani anajua kikao
kilichokaa Zanzibar ni cha ujanjaujanja.’’
Profesa Lipumba alisema ndiye kiongozi wa walinzi wote wa chama,
hivyo wana haki ya kumlinda wanavyotaka wao kwa maslahi ya chama.
Hofu ya Maalim
Alisema Maalim Seif anatakiwa kujiamini na kufika kwenye ofisi hiyo
ili afanye kazi na Mwenyekiti wake za kujenga chama na hakuna kikundi
kilichokuwa kimeandaliwa kufanya vurugu au kugombana na kiongozi huyo.
“Anaweza akaja lakini hawezi kusema kuwa kuna kikundi, hawa ni
walinzi wanaomlinda tangu anagombea nafasi hiyo mwaka 2014, hatuna kikundi ni Blue
Guard na anapaswa kuwaheshimu na si kuwaita kikundi,’’ alisema Lipumba.
Alisema hakuwa na taarifa rasmi ya ugeni wa Maalim Seif, bali
alisikia kwenye vyombo vya habari, kwamba atakuja na wabunge pamoja na wajumbe
kutoka Zanzibar, hivyo alikuwa anasubiri ujio wake kwa kuwa ana ofisi yake.
‘’Maalim Seif ana ofisi hapa, yeye kuja ni jambo la kawaida, ila tangu
nimeanza kufanya shughuli za chama sijamwona ofisini, hana haja ya kutangaza
anaweza akaja ofisini kwa Mwenyekiti wake, apate miongozo ya kazi,’’ alisema.
Kuhusu ujio wa wabunge na wajumbe wa Baraza Kuu alisema
atawajulisha muda wa kukutana, kwa kuwa hajawaita hawapaswi kufika katika ofisi
hiyo kama kikundi.
Alala ofisini
Habari za ndani kutoka ofisi hizo, zilidai kuwa Lipumba alilala
ndani ya ofisi hizo usiku wa kuamkia jana pamoja kundi la wafuasi wake
waliokuwa wakihofia kwamba upande wa Maalim Seif ungefika usiku kuchukua ofisi
yao.
Mmoja wa wafuasi wa Lipumba ambaye alikuwa katika ofisi hizo jana,
alidai baadhi ya wafuasi wa kiongozi huyo walikesha hapo kwa lengo la kumlinda
kwani alikuwa anafanya kazi zake.
‘’Lipumba hakubaki ofisini kwa kuogopa kundi la Maalim Seif ila
alikuwa akifanya kazi zake kwa kuwa ni muda mrefu tangu ajiuzulu hakuwa ofisini
hivyo kazi zimezidi,’’ alisema.
Hata hivyo, Lipumba alikana kulala ofisini bali alifika saa 1:45
asubuhi , ingawa mwandishi wa gazeti hili aliyekuwa katika ofisi hizo muda huo,
hakumwona akiingia na badala yake alielezwa kuwa alikuwa amefika.
Polisi
Katika ofisi hizo magari ya Polisi yalikuwa hayakauki kuanzia saa
moja asubuhi huku Lipumba akieleza kwamba hakuomba msaada wala ulinzi wowote wa
Polisi, kwa kuwa alikuwa ofisini. Juu ya taarifa kwamba Maalim Seif aliomba
ulinzi Polisi, wamsindikize alisema ni jambo la ajabu.
‘’Ikiwa kuna ukweli katika hilo nastaajabu, unaomba ulinzi kwenda
ofisini kwako, ina maana walinzi alionao wa Serikali na wana chama hawatoshi?’’
Alihoji Lipumba.
0 comments:
Post a Comment