*Ni waliotaka kwenda Simiyu kuuzima
*Siku
ambayo anakumbukwa Nyerere
Fidelis
Butahe na Suleiman Msuya
UAMUZI
wa Rais John Magufuli kuagiza viongozi wote wa Serikali walioalikwa sherehe za
Kilele cha Mbio za Mwenge kutohudhuria hafla hiyo ili kubana matumizi,
kimepongezwa na watu wa kada mbalimbali nchini, huku wakihoji sababu za jambo
hilo kutofanyika tangu miaka ya nyuma.
Wamesema
uamuzi huo unaonesha kwamba kiongozi mkuu huyo wa nchi ana lengo la kuinua
uchumi wa Taifa.
Hata
hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro akionesha
wasiwasi kwamba huenda kufutwa kwa sherehe kunatokana na Serikali kukabiliwa na
ukata, aliitaka kuliweka wazi jambo hilo.
Jana
Rais aliagiza viongozi hao walioalikwa kuhudhuria sherehe hizo zinazofanyika kitaifa
kesho wilayani Bariadi mkoani Simiyu, kutohudhuria na kutaka waliokwishalipwa
fedha za posho na safari kwa ajili hiyo wazirejeshe.
Taarifa
iliyotolewa jana Ikulu Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John
Kijazi ilieleza kuwa Rais alitoa maagizo hayo ikiwa ni utekelezaji wa azma ya
Serikali ya Awamu ya Tano ya kubana matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza
rasilimali nyingi katika shughuli za maendeleo ya nchi.
Viongozi
waliotajwa kutakiwa kufuta safari zao za Bariadi ni pamoja na wakuu wote wa mikoa,
wilaya, wakurugenzi wa mamlaka ya serikali za mitaa, mameya na wenyeviti wa halmashauri
za majiji, manispaa, miji na wilaya pamoja na watumishi ambao hufuatana nao
wakiwamo madereva na wasaidizi wao ambao kwa idadi hufikia takribani 1,500.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Kitivo cha Sheria, Dk Onesmo Kyauke alisema uamuzi huo ni sahihi na
kuhoji sababu za kufanyika sasa, wakati Mwenge umekuwa ukizunguka muda mrefu.
Dk
Kyauke alisema fedha hizo zinapaswa zielekezwe katika miradi ya kijamii kwani
inakabiliwa na changamoto nyingi zinazowazunguka.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Lusekelo Kasongwa alisema uamuzi wa Rais na Serikali
ni mzuri na kutakiwa kuungwa mkono.
Kasongwa
alisema hakuna sababu ya jamii kufikiri uamuzi huo unahusu hali ya uchumi
nchini, kwani Serikali ina mambo mengi ya kufanya kuliko sherehe.
“Uamuzi
huo wa Rais ni wa kuungwa mkono, ila jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa uamuzi
huo uoneshe faida yake kwenye jamii,” alisema.
Dk
Jamal Sadick, ambaye ni mtaalamu wa mifupa alisema jitihada hizo zimejikita
kuinua uchumi wa nchi hivyo ni vema jamii ikamwunga mkono na si kulalamika.
“Wapo
watu waliozoea mteremko; safari za mara kwa mara, hivyo kwa sasa hali imekuwa
kinyume najua inawauma, lakini tumpe nafasi abadilishe mfumo na tutafaidi wote,
sidhani kuwa sherehe hizo zina faida ya moja kwa moja kwa jamii,” alisema.
Kwa
kuwa sherehe za kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru huambatana na maadhimisho ya
siku ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere aliyefariki dunia miaka 17 iliyopita,
agizo hilo linawataka viongozi wote wa mikoa na wilaya, kubaki katika maeneo
yao ya kazi na kujiwekea utaratibu wa jinsi ya kuenzi siku hiyo.
Aidha,
Rais aliagiza wilaya zote zilizofanya vizuri kwenye shughuli za maendeleo
wakati Mwenge ukiwa katika maeneo yao, zitambuliwe kwa kutangazwa rasmi katika
kilele cha Mbio za Mwenge na zawadi zilizoandaliwa zitapelekwa kwa wahusika kwa
taratibu utakaoelekezwa na Mamlaka husika kutoa zawadi hizo.
Katika
maelezo yake, Rais alisema kutokana na umuhimu wa Mwenge viongozi wote wa
Simiyu wajitokeze kwa wingi kushiriki sherehe za kuzima Mwenge, ambako mgeni
rasmi atakuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali
Mohamed Shein.
0 comments:
Post a Comment