Hussein Ndubikile
Dk Yahya Msigwa |
SHIRIKISHO la Vyama Huru vya Wafanyakazi
Tanzania (TUCTA) limeitaka Serikali kuharakisha mchakato wa fao la kujitoa kwenye
mifuko ya hifadhi ya jamii ili wafanyakazi wapate haki yao.
Limeitaka pia kuangalia upya makato ya
kodi ya mishahara ili yanufaishe watumishi wote na kueleza kuwa kilichopunguzwa
mwaka jana kinalinda wafanyakazi wachache wa kima cha chini cha mishahara.
Katibu Mkuu wa Tucta, Dk Yahya Msigwa,
alisema hayo kwenye hotuba ya Shirikisho hilo mbele ya Rais John Magufuli
kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika mjini Moshi,
Kilimanjaro jana.
Alisema kwa muda mrefu wafanyakazi
wamekuwa wakisubiri upitishwaji wa fao hilo ambalo litawasaidia kujikimu wanapokosa
ajira huku akiongeza kuwa kiwango cha kodi ya asilimia tisa kinachotozwa kinanufaisha
watumishi wa mshahara wa kima cha chini.
“Tunaiomba Serikali iharakishe kuanzisha
fao la kukosa ajira, ili linufaishe wafanyakazi. Kingine vikokoteo vya mafao ya
mifuko ya jamii viboreshwe ili watumishi waone matunda ya kuchangia,” alisema
Dk Msigwa.
Aliishauri Serikali kufanya maboresho
kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwemo kuunda mifuko miwili wa umma na wa
binafsi ili kuondoa mkanganyiko wa vikokoteo uliopo, wingi wa mifuko ya hifadhi
na kupunguza muda wa wastaafu kusotea mafao.
Alifafanua, kwamba baada ya Serikali
kupunguza kiwango cha kodi ya mishahara (PAYE) kutoka asilimia 11 hadi tisa,
TUCTA imebaini wafanyakazi wanaopokea mishahara ya kima cha chini ndio
wanufaika wakubwa, huku wenye kima cha juu wakiendelea kubanwa.
Kuhusu wawekezaji, Dk Msigwa alisema
wapo wanaokiuka sheria za kazi na kanuni za ajira, ikiwamo kunyima wafanyakazi
haki ya kuunda vyama vya kutetea maslahi yao, pamoja ulipaji mishahara kibaguzi.
Alibainisha kuwa wapo wawekezaji
wanaolipa watumishi wenye Shahada kutoka nje ya nchi Sh milioni saba na
kuwalipa wazawa Sh 700,000.
Aidha, aliiomba Serikali kuzifanyia
maboresho sheria za utumishi wa umma zinazohusu uhusiano wa kazi ili ziwawezeshe
kupeleka masuala yao kwenye Mahakama ya Usuluhishi ya Masuala ya Kazi (CMA).
Pia aliitaka Serikali kuwezesha majaji
kwenda mikoani kumaliza usikilizaji kesi za wafanyakazi kwa wakati na haki
itendeke huku akibainisha kuipunguzia majukumu Wizara ya Kazi, Ajira na Watu
Wenye Ulemavu ili ishughulikie matatizo ya wafanyakazi.
Alisema TUCTA inaipongeza Serikali kwa
kupambana na rushwa, ufisadi, kuondoa watumishi hewa, kupambana na dawa za
kulevya na uboreshaji wa maslahi ya wafanyakazi.
0 comments:
Post a Comment