Dalila Sharif
WAKAZI wa Masaki kata ya Toangoma, Temeke,
wameuomba uongozi kudhibiti matukio ya uhalifu yanayofanywa na kundi la vijana
wanaodhaniwa ni ‘Panya Road’ na kutishia amani, uharibifu wa mali na usalama wao.
Akizungumza Dar es Salaam jana, mmoja wa
wakazi hao, Shamira Ramadhani alisema hali si shwari katika eneo hilo, kutokana
na kuibuka migogoro ya wananchi wa eneo hilo na vijana wasiojulikana wanaochafua
amani ya mtaa huo.
“Takribani wiki ya pili sasa wakazi
hatuna usalama katika maeneo yetu kwa kuogopa kuchomewa moto nyumba zetu,
kutokana na vitisho vya wahuni hawa,” alisema Shamira.
Jack Haule alisema vijana wanaohisiwa
kuwa Panya Rodi hutumia mianya hiyo kuvunja amani pindi mmoja wao anapouawa na
wananchi wenye hasira kali baada ya kuiba mali zao.
“Vijana hawa huvamia maeneo huku wakiwa na
silaha na kupita kwa makundi maeneo ya Masaki na zipo taarifa za kuchoma moto nyumba
mbili kwa petroli na hulipa kisasi cha mwenzao anapouawa,” alisema Haule.
Abdallah Juma alisema Jeshi la Polisi
wilayani humo liko pamoja na wakazi hao wakishirikiana kukabiliana na kukamata
wahalifu hao.
0 comments:
Post a Comment