*Baadhi wadai kashfa ya Escrow, kesi mihadarati vyachangia
*Wengine
wasema ni jambo la kawaida kuachia ngazi wakitaka
Waandishi
Wetu
Rais Magufuli |
WAKATI Rais John Magufuli jana
akitangaza kuridhia maombi ya kuacha kazi kwa majaji wawili na Mkuu wa Mkoa wa
Kilimanjaro, Said Meck Sadiki, wadau wa sheria wamesema huenda kashfa ya Escrow
na dawa za kulevya vinahusika na uamuzi huo.
Ikulu kupitia taarifa ya Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi John Kijazi ilitoa taarifa jana asubuhi ikieleza kuwa pamoja
na Sadiki, Rais aliridhia maombi ya kuacha kazi kwa Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria, Aloysius Mujulizi na Jaji
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Upendo Msuya, kuanzia Mei 15.
Baada ya habari za kuacha kazi kwa
viongozi hao, mijadala ilitawala katika mitandao ya kijamii huku baadhi yao ikihusisha
kuacha kazi kwa Jaji Mujulizi kuwa ni kutokana na kuhusishwa na sakata la
Escrow ambapo alitajwa miongoni mwa majaji walionufaika kwa kupata mgao.
Kwa mujibu wa ripoti ya Bunge kuhusu
sakata la Escrow, Jaji huyo alitajwa kupokea rushwa kwa mmoja wa wamiliki wa kampuni
ya IPTL inayoliuzia umeme Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Wengine waliohusishwa na kashfa hiyo ya
kupokea rushwa ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Profesa Eudes Ruhangisa, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Profesa Anna Tibaijuka.
Wengine
ni aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, na wajumbe wa Bodi
ya Wakurugenzi Tanesco na waliokuwa wenyeviti watatu wa kamati za kudumu za
Bunge, ambao ni Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Victor
Mwambalaswa, Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, William Ngeleja na Kamati ya
Bajeti, Andrew Chenge.
Bunge lilitoa maazimio manane yaliyosomwa
bungeni na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), Zitto Kabwe.
Zitto alisema mabilioni ya fedha yaliyotolewa
kwenye akaunti ya Tegeta Escrow yalitumika kuwapa kinachoonekana kuwa ni
rushwa.
“Vitendo vilivyofanywa na watu hawa
vinaashiria uzembe na makosa mbalimbali ya jinai kama vile wizi, ubadhirifu
kutakatisha fedha haramu, matumizi mabaya ya madaraka, rushwa na kupokea mali
ya wizi,” alisema.
Alitaja azimio la kwanza la Bunge, ni
kulitaka Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama
vichukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.
Zitto alisema watu wote waliotajwa na
taarifa maalumu ya Kamati kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusu miamala
ya Akaunti ya Escrow na watu wengine watakaogundulika baada ya uchunguzi
unaoendelea kuhusika katika vitendo hivyo vya jinai, watachukuliwa hatua
stahiki kwa mujibu wa sheria.
Azimio la tatu ni kuzitaka kamati husika
za kudumu za Bunge, zichukue hatua za haraka na kwa vyovyote vile kabla ya
mkutano wa 18 wa Bunge kuwavua nyadhifa zao za uenyeviti wa kamati husika za
Bunge.
Zitto alitaja azimio la nne kuwa ni la
kumwomba Rais aunde Tume ya Kijaji kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi
ya Jaji Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Kwa upande wa Jaji Msuya uchunguzi wa
JAMBO LEO, kutoka vyanzo mbalimbali unaonesha huenda uamuzi wa kuacha kazi
kwake unatokana na kuhusishwa na uamuzi wa kesi zake za dawa za kulevya, ingawa
taarifa nyingine zinaonesha ugonjwa ndiyo sababu ya hatua hiyo.
Taarifa zinaonesha kwamba Juni 6, 2011
Jaji Msuya alitoa uamuzi wa kuwapa dhamana watuhumiwa wa dawa za kulevya, kwa maelezo
kwamba upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitisha sababu za kuwanyima dhamana,
baada ya kukiri kutowasilisha nyaraka muhimu za kutetea hoja zao.
Mwaka 2013, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam, ilitoa amri ya kukamatwa kwa wadhamini wawili wa raia wa Pakistani
waliokabiliwa na kesi ya dawa za kulevya kukamatwa.
Uamuzi huo huenda una msukumo wa Jaji
Msuya kujiuzulu hasa ikizingatiwa kuwa Rais Magufuli alipata kuzungumzia tabia
za baadhi ya watendaji wa Mahakama kuwaachia watuhumiwa wa kesi za dawa za
kulevya, hivyo kuzorotesha vita hivyo.
Ikumbukwe, kuwa muda mfupi baada ya Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya, Rogers Siyanga kuapishwa
na Rais Magufuli Ikulu, Dar es Salaam, alisema wapo majaji wanaotoa hukumu kwa
kupendelea watuhumiwa hali inayoweka viashiria vya rushwa hivyo kukwamisha mapambano.
“Kazi uliyonipa ni ngumu, kwani
mapambano haya yanahusu watu wenye uwezo. Wakati mwingine wanaharibu kesi, ila
nakuahidi tutahakikisha tunapambana nao wote wanaohusika,” alisema.
Mawakili
Akizungumzia tukio hilo, Wakili wa
Mahakamu Kuu ya Rufaa, Profesa Abdallah Safari alisema ingawa uamuzi huo si wa
mara ya kwanza kufanyika, lakini kwa siku za karibuni unaweza kuonekana ni mpya.
Safari alisema mfumo wa majaji unataka
kuwepo kwa tume ya kuwaondoa ambao unashirikisha nchi za Jumuiya ya Madola,
hivyo inawezekana kulikuwa na fununu ya kufanyika hivyo na wahusika wakaona
waondoke kwa heshima kabla ya hatua ya kuwaondoa kuchukuliwa.
“Ninavyowajua, hao majaji bado ni vijana,
wana nafasi ya kutumikia Mahakama hivyo kwa hayo ambayo yanasemwa kuwa nyuma
yao, yanaweza ndio yamewasukuma kufanya hivyo ili kulinda heshima zao na huko
nyuma wengine walishafanya, sitawataja,” alisema.
Kuhusu uwezekano wa majaji hao kushitakiwa
kama watakuwa wameachia ngazi kwa misingi ya kashfa, alisema kwa mujibu wa
sheria za Mahakama, mtu akifikia sifa ya ujaji analindwa, hivyo hakuna
uwezekano huo.
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika
(TLS), Tundu Lissu alisema jambo hilo ni la kushangaza: “Hili ni jambo jipya
nchini. Huyu Jaji Mujulizi alitajwa kuchota mgawo wa fedha akaunti ya Tegeta
Escrow.
“Alitajwa kuchukua fedha katika akaunti
hiyo. Kwa nini ameacha kazi sijui! Ila kwa vyovyote vile kitendo cha majaji
kuacha kazi licha ya kuwa kinaruhusiwa kikatiba, si cha kawaida sana. Ni vizuri
tukapewa taarifa zaidi juu ya sababu za kuacha kazi,” alisema Lissu.
Kuhusu Jaji Msuya, alisema hawezi
kumzungumzia kwa kina huku akibainisha kuwa kuacha kazi kwa Meck Sadiki kuna
kitu ndani yake.
Lissu alihusisha uamuzi wa Rais Magufuli
kumhamishia Kilimanjaro kutoka Dar es Salaam, huku nafasi yake ikichukuliwa na
mteule mwingine wa Rais ambaye awali alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni.
Lissu alibainisha kuwa TLS itatoa
taarifa rasmi ya kuacha kazi kwa majaji hao baada ya kusoma taarifa ya Ikulu na
kufanya uchambuzi wa kina.
Wakili
wa kujitegemea, Kaloli Mluge alisema hajui ni sababu gani ambayo imefanya
majaji hao waache kazi, lakini yeye anadhani maslahi yamepungua na pia ajira
serikalini imekuwa ngumu, tofauti na kipindi cha nyuma.
Mluge
alisema hivi sasa watu wamechoka kufanya kazi kwa kuburuzwa, kila mtu anafahamu
taaluma yake inamtaka afanye nini, kwa hiyo hakuna sababu ya kuanza kumfundisha
kazi wakati anajua majukumu yake.
“Ni
ngumu kuusemea moyo, lakini mzee kabana sana, maisha yamekuwa magumu serikalini
hakuna mtu anayetamani kufanya kazi naye, kutokana na mfumo anaotumia wa
kuwafundisha watu wafanye nini,” alisema Mluge.
Wakili
Emmanuel Muga alisema njia waliyotumia majaji hao kuacha kazi ni sahihi na pia
si jambo la ajabu.
Alisema
kila mtu ana uhuru wa kuacha kazi pasipo kuulizwa maswali mengi, kwa sababu
hawana makosa na kama wameamua kufanya hivyo ni sawa. Inawezekana wameamua
kufanya kazi ya uwakili, ambalo ni jambo zuri tu.
Wakili
Abubakar Salim alisema si mara ya kwanza majaji kuacha kazi, watu wamehamaki
kwa sababu huko nyuma kulikuwa hakutolewi taarifa ndiyo maana limeonekana kama
suala geni.
“Wapo
waliokuwa wakiacha kazi kwa uamuzi wao wa kupumzika na kuendelea na maisha
mengine. Hii ya leo imeleta maswali mengi kwa sababu tu watu wameona ni tukio
jipya, lakini mambo hayo yapo, sema yalikuwa hayatolewi taarifa,” alisema.
Wakili
Jamhuri Johnson alisema si jambo geni na kuwa ugeni wake ni kutangazwa katika
vyombo vya habari, kitu ambacho huko nyuma hakikufanyika ila sababu za kuacha
hawa hatujui.
“Hapa
upya ni kutangazwa, lakini majaji wengi wameacha kazi kwa mfano Jaji Chingwile
alikuwa Kilimanjaro aliacha kazi, Jaji Kalegea wa Mahakama ya Rufaa aliacha
kazi, tatizo ni kutangaza ndicho naona,” alisema.
0 comments:
Post a Comment