*Wasomi wadai vilio vya wananchi vimeongezeka
Waandishi Wetu
Rais John Magufuli |
SERIKALI ya Awamu ya Tano imefanya
vizuri tangu ilipoingia madarakani, ikifanikiwa pamoja na mambo mengine kurejesha
nidhamu ya kazi na kuwajibisha viongozi na watumishi wa umma.
Aidha, imeanza utekelezaji wa miradi
mikubwa ya kiuchumi ikiwamo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa,
ununuzi wa ndege, kuzuia matumizi yasiyo ya lazima na kufuta maadhimisho ya
sherehe mbalilimbali ni baadhi ya mambo yaliyofurahiwa na wengi.
Hata hivyo, wakati Serikali hiyo
inayoongozwa na Rais John Magufuli ikikaribia kumaliza mwaka wa pili, baadhi ya
wasomi na wanasiasa wametaja mambo 10 yanayotakiwa kufanyiwa kazi kutokana na
utekelezaji wake kuathiri kundi kubwa la Watanzania wakisema yanaweza kumweka
mtegoni.
Wamesema licha ya kuwa baadhi ya mambo
hayo yamefanyika kwa nia njema, utekelezaji wake ulikuwa na kasoro, huku
wakikosoa baadhi ya kauli, hatua sambamba na kufanyika mambo waliyosema hayana
ulazima kwa sasa.
“Matukio hayo yana maana kubwa sana
kwani wananchi wamejawa na hasira hakika wanahifadhi hasira zao kuelekea mwaka
2020,”alisema Zitto Kabwe, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo na Mbunge wa
Kigoma Mjini.
Mambo kumi yanayomweka JPM mtegoni
Mikutano ya hadhara
Marufuku ya mikutano ya siasa mpaka
wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2020 kama ilivyotangazwa na Rais
Magufuli ni moja kati ya uamuzi ulioathiri wanasiasa na vyama, hasa vya
upinzani.
Sababu iliyotolewa na Rais Magufuli ni
kuwa huu ni muda wa kufanya kazi na siyo siasa. Katika kufafanua kauli yake,
Rais alisema wabunge na madiwani tu ndiyo wanaoruhusiwa kufanya mikutano katika
maeneo yao na hawaruhusiwi kuleta wageni kutoka nje.
2. Bomoabomoa
Mwanzoni mwa utawala wake liliibuka
zoezi la kuondoa watu waliojenga katika maeneo yasiyoruhusiwa.
Bomoabomoa hiyo iliendeshwa na Baraza la
Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar
es Salaam na kuathiriwi watu wengi masikini ambao ndiyo waliomchagua pia Rais
huyo wa Awamu ya Tano.
Zoezi hilo lililenga nyumba zilizojengwa
mabondeni, kwenye fukwe za bahari ya Hindi, kingo za mito na maeneo ya wazi na
hivi karibuni wamebomolewa waliojenga pembezoni mwa reli ya kati.
3. Matangazo ya Bunge ‘live’
Kusitishwa kwa urushwaji wa matangazo ya
Bunge moja kwa moja nao umewagusa baadhi ya wananchi ambao tangu kutolewa
katazo hilo wamekuwa wakilipinga licha ya kuwa baadhi ya televisheni hurekodi
na kurusha usiku.
Machi mwaka huu chombo kimoja cha habari
kiliandika kuwa Rais Magufuli katika kikao chake cha ndani na wabunge wa CCM
mjini Dodoma, aliwaeleza kuwa yeye ndiye aliyeamua kusitisha mikutano ya Bunge
kuoneshwa moja kwa moja katika televisheni.
4. Wabunge wa CCM kutowatembelea wa
upinzani
Katika kikao hicho pia iliripotiwa jinsi
Rais Magufuli alivyoshangazwa na hatua ya baadhi ya wabunge wa CCM waliounda
kamati ya kutaka kwenda kumtembea mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless
Lema alipokuwa gerezani jambo alilolifananisha na usaliti kwa chama chake.
Lema alikaa gerezani kwa muda wa miezi
minne kwa kukosa dhamana kutokana na mashtaka yaliyokuwa yakimkabili. Kauli
hiyo ambayo haijakanushwa popote ilizuia taharuki huku wasomi waliotoa maoni
katika gazeti hili wakitofautiana mtazamo wao.
5. Utumbuaji majipu
Baada ya kuapishwa Novemba 5, mwaka 2015
Rais Magufuli alianza utekelezaji wa majukumu yake kwa mfumo wa kuwajibisha
watendaji wazembe, wala rushwa na wanaolisababishia Taifa hasara kwa njia
mbalimbali. Mfumo huo wa utendaji kazi umejipatia umaarufu kuwa ‘utumbuaji
majipu’.
Licha ya utumbuaji huo kuungwa mkono,
wapo walioukosoa wakitaka watakaotumbuliwa wawe watu waliobainika kuwa na
makosa na kasoro mbalimbali, ukiwakumbe hadi watumishi wasiohusika.
Tangu kuanza kwa utumbuaji, zaidi ya watumishi
1,000 wameshatumbuliwa jambo linalowafanya katika maisha yao kutosahau utawala
wa Serikali ya Awamu ya Tano.
6. Kufuta safari za nje
Uamuzi wa Rais kubana matumizi, ikiwa ni
pamoja na kudhibiti ziara za nje zisizo na tija, safari za mafunzo nje ya nchi,
warsha, semina, makongamano na matamasha ulisifiwa na kada mbalimbali nchini
lakini kwa kiasi fulani uliacha simanzi kwa watumishi, hasa waliokuwa wakitumia
maeneo hayo kujipatia fedha za bure.
7. Pesa kutoweka, kupunguzwa kazi
Wapo wanaofurahia hatua za Serikali
kuthibiti na kubana matumizi, lakini uamuzi huo umeathiri sekta nyingi kutokana
na fedha kutoweka.
Si hoteli, baa, mashirika ya usafiri,
kampuni za huduma za chakula, vyombo vya habari wala viwanda zilizoepuka athari
za uamuzi huo wa Serikali.
Katika kipindi cha utawala wa awamu ya
tano, ulioshuhudia fedha kutoweka baadhi ya mashirika na taasisi hasa binafsi
zililazimika kupunguza wafanyakazi wake, huku baadhi ya wafanyabiashara
wakifunga biashara kutokana na mzunguko wa fedha kuwa hafifu wakilazimika
kufanya hivyo ili kwenda sambamba na uzalishaji na kupata faida.
8. Vyeti feki
Uhakiki wa vyeti unaofanywa na Serikali
kwa kiasi kikubwa umeacha alama nyingine kwa Watanzania. Baada ya kupokea
majina 9,932 kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Umma na
Utawala Bora), Rais Magufuli aliagiza wote waliotajwa kughushi vyeti waondoke
vituo vya kazi kabla ya Mei 15 na watakaokaidi watafikishwa mahakamani.
Pengine sio ajabu kutajwa kwenye orodha
hiyo kwa kuwa ukaguzi haukuacha mtu au cheo, lakini kugundulika kwake kunaibua
maswali zaidi katika uhakiki huo ambao tayari uemshaonyesha dosari kama kutaja
majina ya baadhi kuwa wana vyeti vya kughushi vya elimu ya sekondari wakati
hawakuviwasilisha kwenye uhakiki uliofanyika.
9. Tetemeko la ardhi Kagera
Septemba 11 mwaka jana mikoa ya kanda ya
ziwa ilikumbwa na tetemeko la ardhi ambako watu takribani 17 walipoteza maisha,
huku zaidi ya nyumba 840 zikibomona na nyingine 1,264 kuharibika.
Wakati akipokea taarifa ya maafa hayo,
Rais Magufuli alisema Serikali itarekebisha miundombinu iliyoharibiwa na
tetemeko na kuwataka waliobomolewa nyumba, wajipange kuzirekebisha.
Serikali ilizuia watu au taasisi kutoa
misaada kwa waathirika, badala yake ikaagiza wapiti Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huku kipaumbele kikiwa ni kukarabati
miundombinu jambo ambalo lilipingwa na kulalamikiwa na watu waliotaka fedha
hizo ziende moja kwa moja kwa waathirika.
10. Kudhibiti mihimili
Licha ya Seriklai kuwa na wajibu wa
kutafuta fedha, kitendo cha Mahakama na Bunge kuwa mihimili inayojitegemea
lakini kujikuta ikipangiwa mambo kadha wa kadha na Serikali kumezungumziwa na
wachambuzi wa masuala mbalimbali nchini kuwa si utaratibu mzuri.
Mfano ni uamuzi wa Rais kuagiza fedha za
sherehe ya kuwapongeza wabunge kutumika kununulia vitanda Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH).
Maoni ya wasomi, wanasiasa
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Abdallah Safari alisema suala la
kuzuia mikutano ya hadhara na kutokuonesha Bunge ni moja ya mambo ambayo
yanaweza kumnyima Rais Magufuli nafasi ya kutetea kiti chake.
“Rais anasema hakuna siasa na wananchi
wafanye kazi lakini anashindwa kuelewa kwamba kuwaminya huko na kuwatengenezea
watu hofu ya kushindwa kuzungumza kunawafanya wazidi kuwa majasiri na siku
wakipata nafasi ya kufanya maamuzi katika chumba cha kura basi hawatomchagua,”alisema.
“Uhusiano wake na wananchi umedorora kwa
kuwa anawafanya wawe kimya na hofu lakini akae akijua kuwa 2020 watu
wataikimbia minyororo kwa kuwa anasema analeta maendeleo lakini utekelezaji
hakuna na watu wakijaribu kumkosoa wanatishwa na kukamatwa.”
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu
Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema inawezekana Rais akabadilika baadayee
kwa kuwa kisiasa bado miaka ni mingi kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Mbunda alisema mbali na mambo hayo,
suala la ukata kwa wananchi walio wengi ndio limegeuka ajenda huku akitolea
mfano jinsi anavyozungumzia hovyo katika mitandao ya kijamii.
“Nadhani demokrasia inawapa nguvu wananchi kuliko viongozi kwa kuwa wao ndio
wanaochagua lakini hapa kwetu viongozi walio wengi huwa wanyenyekevu pindi
wanapoomba kura lakini wakishapata madaraka huwasahau wapiga kura wao,”alisema.
“Kuna mambo mengi yanaweza kukwamisha
safari yake 2020 mfano suala la kuonekana kutojali wananchi wake ukirejea kauli
yake wakati wananchi wakilalamika njaa, chakula hakuna yeye akawaambia Serikali
haitoi chakula hiyo maana yake Serikali haijali.”
Mhadhiri mwingine wa chuo hicho, Dk
Onesmo Kyauke alikuwa na mtazamo tofauti kuwa mambo hayo hayawezi kuwa sababu
ya Rais Magufuli kurudi madarakani lakini akaonya kuwa anapaswa kubadilika ili
kurudisha imani ya wananchi waliyokuwa wamejenga kwake.
“Mfano suala la Bunge Live ni haki ya
Wananchi karibu nchi zote duniani wanonesha Bunge, ni jambo la hatari kuwanyima
watu haki zao za msingi, hata kama Sheria haisemi lioneshwe lakini Sheria hiyo
hiyo haikatazi Bunge Live,”Alisema Dk Kyauke.
Mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini, David
Kafulila alitaja uamuzi wa kufuta mikutako ya hadhara, kubainisha kuwa jambo
hilo litampa wakati mgumu Rais Magufuli kwenye uchaguzi mkuu wa 2020.
“Pia kuzuia
mikutano ya Bunge ni dosari kubwa kwake, katika utawala wake kuna ukiukwaji wa
haki za binadamu, kukandamiza demokrasia na kutunga sheria kandamizi,”alisema
Kafulila na kubainisha suala la vyeti feki ni sahihi kufanyika.
0 comments:
Post a Comment