BENKI ya Dunia (WB) imekubali kusaidia utekelezaji
wa sera ya elimu bila malipo kwa Serikali ambapo imetoa dola milioni 80 sawa na
Sh bilioni 181.
WB imefikia uamuzi huo baada ya kuona
mwitikio mkubwa wa wanafunzi kujiunga na shule za msingi, hali inayoonesha
kuanza kuilemea Serikali kutoa elimu hiyo kuanzia shule ya msingi hadi kidato
cha nne.
Mkurugenzi Mkaazi wa WB kwa Tanzania,
Somalia, Malawi na Burundi, Bella Bird alibainisha jana kwamba fedha hizo zimetolewa
na taasisi ya International Development Association (IDA) inayokwenda na mpango
wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
“Lengo ni kusaidia Serikali kukabiliana
na changamoto inazokutana nazo katika mpango huo wa kutoa elimu bila malipo,”
alisema.
Alisema pia lengo la lingine la kutoa
fedha hizo ni kusaidia kuhudumia ongezeko la watoto wanaoijunga na shule pamoja
na elimu bora itakayosaidia Taifa baadaye.
“Mpango wa elimu bila malipo ni jambo la
kusaidia Serikali kufikia malengo ya kuwapa watoto wa kitanzania elimu, hivyo
sisi WB tumeamua kuongeza nguvu ili Serikali isikwame,” alisema.
Bird aliipongeza Serikali kuondoa
vikwazo katika utoaji elimu, hivyo kusababisha makundi yote kupata elimu bila
tatizo lolote.
Mkurugenzi huyo alisema ni dhahiri uamuzi
huo utasababisha ubora wa elimu huku dhana ya utekelezaji lengo la elimu kwa
wote ikikamilika, kwa kuwa hakuna atakayeachwa nyuma.
“Tunaamini kuwa kupitia msaada huu, ni
matumaini yetu kuwa Mamlaka itahakikisha kuwa watoto wanapata elimu hasa ambao
wanaishi katika mazingira magumu,” alisema.
Alisema mpango huu ulianza mwaka 2014
ambapo WB ilipitisha dola milioni 122 ili kuhakikisha kuna elimu bora kwa shule
za msingi na sekondari.
Msaada huo wa WB ni mwendelezo wa benki
hiyo kutoa misaada kwa nchi ambapo hivi karibuni Rais wake, Dk Jim Yong Kim alizuru
nchini na kuweka jiwe la msingi la daraja la juu Ubungo, Dar es Salaam ambao
utagharimu zaidi ya Sh bilioni 188.71 msaada kutoka benki hiyo.
Aidha, WB hadi sasa inafadhili miradi
zaidi ya 28 nchini ukiwamo ujenzi wa barabara ya mwendo kasi kwa gharama ya
zaidi ya dola bilioni 4.2 ambapo Tanzania itarudisha kwa riba ndogo ya asilimia
0.5.
0 comments:
Post a Comment