Mwandishi Wetu
Nape Nnauye |
BAADA ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam
kusema aliyekuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape
Nnauye, hakuwa na mamlaka ya kuunda kamati kuchunguza tukio lake la kuvamia
kituo cha Clouds Media, wanasheria nchini wamesema kiongozi huyo anapotosha
umma.
Wamesema kauli ya Mkuu huyo wa Mkoa kuwa
ana mamlaka sawa na waziri kutokana na kuteuliwa na Mamlaka moja ya uteuzi si
sahihi, wakibainisha kuwa licha kuwa wakuu wa mikoa huteuliwa na Rais kama ilivyo
kwa mawaziri, Nape aliunda kamati kuchunguza tukio lililotokea katika eneo
linalosimamiwa na wizara yake, na si kuchunguza mwenendo na utendaji kazi wa Mkuu
wa Mkoa.
Kiongozi huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam
alitoa kauli hiyo juzi, wakati akihojiwa na kituo cha luninga cha Star Tv kwenye
kipindi cha Tuongee Asubuhi, huku akikwepa baadhi ya maswali kuhusu elimu yake
na jina lake halisi kwa kivuli cha “kuandamwa na wauza dawa za kulevya”.
“Hata kwa akili ya kawaida tu, unaweza kutofautisha
mamlaka zao. Mkuu wa Mkoa ni kiongozi wa mkoa tu, ila waziri ni kiongozi wa
nchi nzima kwa eneo analosimamia au kuongoza,” alisema Profesa Abdallah Safari.
Katika kipindi hicho, Bashite aliponda uamuzi
wa Nape kuunda kamati ya kumchunguza baada ya kuvamia ofisi za Clouds Tv, akiwa
na askari wenye silaha za moto na kulazimisha sehemu ya kipindi cha Shilawadu
kurushwa hewani.
“Matukio kama haya hutokea nchi
inapotaka kupinduliwa, lakini kama Rais yupo na nchi haijapinduliwa, basi
kuingia ndani ya chombo cha habari na silaha, huku ni sawa na kunajisi uhuru wa
habari,” alisema Nape.
Wakati akipokea ripoti ya kamati hiyo
baada ya kupita saa takribani 24, Nape alisema ataifikisha kwenye Mamlaka za Uteuzi
juu yake kwa maelezo kuwa yeye hana mamlaka ya kumchukulia hatua Mkuu wa Mkoa.
Hata hivyo, Nape aliachwa katika
mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais John Magufuli saa
12 baada ya kupokea ripoti hiyo iliyokuwa na timu ya watu sita.
Wanasheria
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Dk James Jesse alisema: “Nape hakuandaa mamlaka ya kumchunguza Makonda,
yeye alichunguza jambo lililotokea katika wizara yake, alichunguza jambo si
mtu.
“Kama angemchunguza Mkuu wa Mkoa, kweli
angekuwa hana mamlaka hayo. Lile ni tukio na ili upate picha ni lazima uhoji
watu wote ambao walihusika kwenye hilo tukio,” alisema.
Kuhusu mamlaka zao, alisema: “Katiba
haisemi kuhusu mamlaka, lakini ukitazama tu, mmoja anaongoza wizara ambayo ni
mamlaka ya kitaifa na huyu mwingine anaongoza mkoa. Hivi utasema wote
wanalingana kwa mamlaka kweli?”
Alisema ukubwa au mamlaka ya kiongozi
hayatokani na ukubwa wa bajeti aliyonayo katika eneo analoongoza, “watu
huangalia unaongoza mkoa, wilaya au wizara.”
Katika ufafanuzi wake, Profesa Safari alisema:
“Kazi zao zinatofautiana sana. Waziri ni wa nchi nzima na mkuu wa mkoa ni wa
mkoa tu. Waziri ni mjumbe wa Baraza la Mawaziri na katika kutekeleza wajibu
wake, waziri ana wajibu wa kuunda tume kuchunguza jambo chini ya wizara yake.”
Aliongeza: “Kama huyo mkuu wa mkoa hataki
kukubali kuhusu mamlaka ya waziri sijui anawaza nini, maana hili liko wazi na
wanasheria tumelieleza kiundani zaidi. Kama hatambui hilo anashangaza, huko ni
kujinyanyua tu.”
Alisema Nape alikuwa na lengo la kutaka
kujua ukweli wa tukio lililotokea Clouds Tv, na si kumchunguza mkuu wa mkoa.
Mhadhiri mwingine wa Chuo hicho, Dk
Onesmo Kyauke huku akichambua sheria inayoongoza utendaji katika mikoa (The
Regional Administration Act), alisema waziri anaweza kutoa mapendekezo dhidi ya
mkuu wa mkoa kwa Mamlaka ya Uteuzi ambayo ni Rais.
“Kama
mkuu wa mkoa akifanya kosa, nafikiri waziri anapaswa kuwasilisha malalamiko
yake kwa Rais… mkuu wa mkoa anashughulikia mkoa wake tu, lakini waziri
anashughulikia majukumu yanayohusu wizara yake kitaifa, yaani nchi nzima, ila tatizo
ni kuwa mkuu wa mkoa hayuko chini ya waziri.”
Katiba
Kwa mujibu wa Ibara ya 61 (2) ya Katiba
ya Tanzania; wakuu wa mikoa Tanzania Bara watateuliwa na Rais baada ya
kushauriana na Waziri Mkuu.
Kifungu kidogo cha (4) kinasema; Bila kuathiri masharti
ya ibara ndogo ya (5), kila Mkuu wa Mkoa, atakuwa na wajibu wa kusimamia
utekelezaji wa kazi na shughuli zote za Serikali ya Jamhuri ya Muungano katika
mkoa aliokabidhiwa; na kwa ajili hiyo, atatekeleza kazi na shughuli zote
zilizotajwa na sheria, au kwa mujibu wa sheria kama hizi au shughuli za mkuu wa
mkoa na atakuwa na madaraka yote yatakayotajwa na sheria yoyote iliyotungwa na
Bunge.
Mawaziri
Ibara
ya 55 (1) inasema; Mawaziri wote ambao ni wajumbe wa Baraza la Mawaziri kwa
mujibu wa ibara ya 54 watateuliwa na Rais baada ya kushauriana na Waziri Mkuu.
Kifungu
kidogo cha (2) kinasema; Pamoja na mawaziri waliotajwa katika ibara ndogo ya
(1), Rais aweza, baada ya kushauriana na Waziri Mkuu, kuteua naibu mawaziri.
Naibu mawaziri wote hawatakuwa wajumbe wa Baraza la Mawaziri.
(3)
Rais aweza kuteua idadi yoyote ya naibu mawaziri ambao watawasaidia mawaziri
katika utekelezaji wa kazi na shughuli zao. (4) Mawaziri na naibu mawaziri wote
watateuliwa kutoka miongoni mwa Wabunge.
(5)
Bila kujali masharti ya ibara ndogo ya (1), ikitokea
kwamba
Rais anahitajika kuteua waziri au naibu waziri baada
ya
Bunge kuvunjwa, basi aweza kumteua mtu yeyote ambaye
alikuwa
mbunge kabla ya Bunge kuvunjwa.
0 comments:
Post a Comment