Suleiman Msuya
KAMPUNI ya Simu ya Airtel na Shirika la
Elimu, Sayansi na Utamaduni Duniani (Unesco) wameazimia kushirikiana kuinua uchumi
na kuboresha elimu kwa kutumia redio za kijamii.
Meneja wa Huduma za Jamii wa kampuni
hiyo, Hawa Bayumi alisema kuwa ushirikiano huo utazifanya redio hizo kutumia
minara ya Airtel kurusha matangazo yake, kutoa huduma za intaneti na huduma za
fedha.
Bayumi alibainisha kuwa ushirikiano huo
utazihusisha redio tisa za maeneo mbalimbali nchini.
Alizitaja redio zitakazonufaika kuwa ni Radio
Fadeco ya Kagera, Kyela FM (Mbeya), Pangani FM (Tanga), Kahama FM (Shinyanga),
Uvinza Radio (Kigoma), Sengerema Radio (Mwanza) na Loliondo Radio ya Arusha
huku Mtegani FM ya Zanzibar na Micheweni ya Pemba zikiwa bado hazijajihusisha
na mpango huo kikamilifu.
“Mpaka sasa ushirikiano huu ushafikia
jumla ya redio saba na kwa kutumia minara ya Airtel ambayo iko kwenye maeneo
yao, redio hizi zimeweza kuboresha ubora wa matangazo na kufikia maeneo mengi
na wasikilizaji wengi, alisema Bayumi,” alisema.
Katika kuboresha elimu pamoja na kuinua
hali ya kiuchumi, Meneja Miradi UNESCO, Nancy Kaizilege alisema shirika hilo
linasaidia redio za kijamii kwa kuwajengea uwezo watangazaji pamoja na waandaji
wa vipindi kwa huduma bora na pia kuweka mkazo kwenye elimu ya haki za
kibinadamu.
Alisema wamekuwa wakisisitiza habari
zinazohusu watu wenye ulemavu wa ngozi, changamoto za uzazi na elimu ya uzazi
wa mpango, elimu kuhusu maambukizi ya virusi vya ukimwi pamoja na kumwezesha mtoto
wa kike.
Kaizilege alisema pia vipindi vyenye
kujadili heshima ya mwanamke kwenye jamii jambo ambapo kwa kiasi kikubwa limesaidia
kupunguza ndoa za utotoni.
“Tumeshuhudia siku za karibuni radio
hizi zikileta wadau mbalimbali pamoja na kufanikisha miradi mikubwa ya
maendeleo kwa mfano wilaya ya Kahama imeweza kujenga na kuboresha miundombinu
ya barabara kwa kushirikiana na migodi ya uchimbaji madini,” alisema.
0 comments:
Post a Comment