Mwandishi Wetu
IGP Simon Sirro |
MUDA mfupi baada ya kuapishwa Ikulu Dar
es Salaa, Mkuu wa Jeshi la Polisi mpya, IGP Simon Sirro, amesema uhalifu hauwezi
kupungua kwa kulitegemea jeshi hilo pekee, bali nguvu ya pamoja inahitajika
akitoa mwito kwa wananchi kushirikiana na jeshi lake.
Amesema wananchi wakitoa taarifa za
wahalifu waliopo maeneo yao jambo hilo litaweza kupunguza au kuondoa uhalifu
nchini.
Aidha, IGP Sirro ametaja kipaumbele
chake cha kwanza kuwa ni kupambana na uhalifu na kudhibiti nidhamu kwa askari
akieleza bila hivyo itakuwa vigumu kumaliza uhalifu, huku akiwaahidi kulala
usingizi wa amani wananchi wa Mkoa wa Pwani kwa kufanyia kazi matukio ya
uhalifu yaliyojitokeza.
Alisema hayo jana alipokuwa akizungumza
na waandishi wa habari baada ya kuapishwa na Rais John Magufuli kuliongoza Jeshi
la Polisi la Tanzania.
“Uhalifu hauwezi kupungua kwa kutegemea
Jeshi la Polisi pekee, tunahitaji nguvu ya pamoja ili kushinda vita hiyo,
ushirikiano wa wananchi unahitajika kwa kiasi kikubwa,” alisema IGP Sirro.
Akiwa IGP wa kumi kuongoza jeshi hilo,
Sirro alisema kazi kubwa ya Jeshi la Polisi ni kulinda na kuhakikisha usalama
wa raia na mali zao na kwamba ni wajibu wa jeshi lake kuhakikisha Taifa lina
ulinzi wa kutosha utakaowezesha wananchi kuishi kwa amani na utulivu wakifanya
kazi zao bila kubugudhiwa.
“Kipaumbele cha kwanza katika utendaji
wangu ni kupambana na uhalifu pamoja nidhamu ya watendaji kazi kwani bila
nidhamu, kazi ya kupambana na wahalifu haiwezi kufanikiwa,”alisema IGP Sirro.
Akizungumzia matukio ya uhalifu ya mara
kwa mara yaliyoambatana na mauaji mkoani Pwani, IGP Sirro alisema atafanyia
kazi changamoto zinazowakabili na kuhakikisha wananchi wake wanaishi kwa amani
na utulivu.
IGP Sirro ambaye kabla ya uteuzi huo,
alikuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, alimshukuru Rais
Magufuli kwa kumuamini na kumteua kushika nafasi hiyo akiahidi kufanya kazi kwa
bidii na uadilifu.
Kabla ya uteuzi huo, Sirro aliwahi kuwa Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mwanza, kisha Kamanda wa Kikosi cha Operesheni Maalum.
0 comments:
Post a Comment