Mary Mtuka
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu |
WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, imelaani kitendo cha mkazi wa kata ya Rudete mkoani
Geita, ambaye ni mama wa kambo, kumchoma moto mtoto wa miaka mitatu akituhumiwa
kuiba chakula alichoachiwa baba yake.
Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo
vya habari Dar es Salaam jana, Wizara ilisema tukio hilo linakinzana na
kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia mwaka huu, ambayo
pamoja na mambo mengine, inasisitiza wazazi na walezi, kutekeleza wajibu wao wa
kuimarisha malezi kwa ajili ya ustawi wa watoto katika familia na jamii kwa jumla.
"Katika kutekeleza utoaji haki za mtoto
na ustawi wake, wadau wanaotoa huduma kwa mtoto wanasisitizwa
kusimamia upatikanaji wa haki zote za msingi katika familia na jamii, ikiwamo
haki ya kuishi, kulindwa, kuendelezwa, kushirikishwa na kutobaguliwa,"
ilieleza.
Wizara inawataka wananchi kutoa
ushirikiano wa kufichua wanyanyasaji dhidi ya watoto kwa kutoa taarifa kwenye Mamlaka
husika, ili wahusika wa ukatili wachukuliwe hatua.
Aidha, Wizara ilitoa maelekezo kwa
maofisa maendeleo na ustawi wa jamii kuhakikisha mtoto huyo anapewa huduma ya
matibabu haraka ili kumrejesha katika afya njema.
“Hata hivyo kwa kuwa jukumu la ulinzi na
usalama wa mtoto linatekelezwa kwa ushirikiano mkubwa na Polisi, tunaamini suala
hilo linafuatiliwa kuhakikisha watuhumiwa wa vitendo vya ukatili na unyanyasaji
dhidi ya huyo mtoto wanapatikana," ilisema taarifa.
0 comments:
Post a Comment