Jacquiline Mrisho, Maelezo
Profesa Samweli Manyele |
TANZANIA imeshika
nafasi ya tatu barani Afrika baada ya Afrika Kusini na Nigeria kwa kuwa na
Sheria bora ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali.
Kauli hiyo
imetolewa juzi Dar es Salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Profesa Samweli
Manyele, alipozungumza na waandishi wa habari juu ya mkutano wa Kimataifa wa
Udhibiti wa Kemikali na Kemikali Taka uliofanyika Geneva, Uswisi Aprili 24 hadi
Mei 5 mwaka huu.
Profesa Manyele
amesema kuwa katika Bara la Afrika Tanzania ndio nchi pekee ambayo ina taasisi
ya Serikali inayosimamia kemikali wakati nchi zingine usimamizi wa masuala ya
kemikali upo katika taasisi za mazingira kitu ambacho kinapelekea usimamizi
hafifu wa kemikali hizo.
“Tanzania ni nchi
pekee Afrika ambayo taasisi inayohusika na masuala ya kemikali ipo chini ya
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na pia ni taasisi
yenye kusimamiwa na wataalamu wa kemikali waliobobea pamoja na kuwa na maabara
kubwa inayojulikana kimataifa,”alisema Prof. Manyele.
Akiongelea
kuhusu mkutano huo, Prof. Manyele amesema kushiriki katika mkutano huo ni jambo
la kisheria hivyo kupeleka watumishi watatu kutoka kwenye taasisi hiyo
inadhihirisha kuwa Tanzania imetimiza majukumu yake kama Taifa.
Amefafanua kuwa
mkutano huo unaisaidia taasisi kutoa taarifa kuhusu utendaji kazi, kujifunza
nchi zingine wanafanyaje kazi zao, kupata majibu ya moja kwa moja pamoja na
kujadiliana namna ambavyo wataboresha utendaji kazi.
Kwa upande wake
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Huduma ya Ubora wa Bidhaa, Daniel Ndiyo ametaja wadau
wanaotakiwa kupata taarifa na maamuzi ya mkutano huo kuwa ni wafanyabiashara,
watumiaji wa kemikali hizo pamoja na mamlaka mbali mbali za usimamizi wa
kemikali.
Meneja wa Kanda
ya Kaskazini GCLA , Christopher Anyango amesema mkutano huo unawasaidia
wananchi kupata msaada wa haraka kutoka katika Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali
kwa kuwa wana uelewa pamoja na kupata mafunzo ya kemikali zinazoruhusiwa na
zisizoruhusiwa kulingana na mahitaji kwa wakati husika.
Maabara ya
Mkemia Mkuu wa Serikali ilishiriki katika mkutano huo wa utekelezaji wa
mikataba mitatu ikiwemo ya usafirishaji wa taka sumu kimataifa (Basel), mkataba
unaohusu kemikali zenye madhara na zinazochukua muda mrefu kuoza katika mazingira
(Stockholm) pamoja na mkataba wa Rotterdam unaohusu upashanaji taarifa juu ya
kemikali hatari na viuatilifu katika biashara ya kimataifa.
0 comments:
Post a Comment