Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Ndege ya Tanzania (ATCL),
imeanzisha safari za kutoka Tabora kwenda mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam ikiwa
na lengo la kurahisisha huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo kwa mikoa
hiyo na ile ya jirani.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Edwin Ngonyani alisema katika uzinduzi wa huduma hiyo kuwa
kuanzishwa kwa safari hizo kutaongeza wigo wa biashara na kukuza uchumi kupitia
sekta mbalimbali ikiwemo utalii na
kilimo.
“Naamini wakazi wa mkoa wa Tabora na
mikoa ya jirani, sasa mtanufaika kwa ujio wa ndege hii, matumaini yangu kwamba
mtatumia usafiri huu kurahisisha shughuli zenu za kibiashara na kijamii,”alisema.
Ngonyani aliwataka wananchi wa Mkoa wa
Tabora kutumia fursa ya ujio wa ndege hiyo kama chachu ya kuleta maendeleo
katika mkoa huo.
Sambamba na hilo, Ngonyani alisema katika
kuhakikisha usafiri wa anga unaimarika nchini, Serikali itaongeza ndege
nyingine tatu katika mwaka wa fedha 2017/18 ambapo hadi kufikia mwezi Julai mwakani
ndege hizo zitakuwa zimewasili.
Katika hatua nyingine, Ngonyani
amewaagiza wafanyakazi wa ATCL kufanya kazi kwa juhudi, uadilifu na weledi ili
kuijengea sifa kampuni hiyo na kuvutia wateja ili kujiimarisha katika soko la
ushindani.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo (Sekta ya
Uchukuzi), Dk. Leonard Chamuriho aliwataka wananchi wa mkoa huo kutumia fursa
ya kupata usafiri wenye gharama nafuu na wa muda mfupi.
Mkuu wa Mkoa huo, Aggrey Mwanri aliwataka
wananchi wa mkoa huo na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kutumia huduma za
usafiri huo waliokuwa wakiusubiri muda mrefu.
0 comments:
Post a Comment