Grace Gurisha
WAKATI kukiwa na mkanganyiko kuhusu wapi walipo watuhumiwa wa dawa za kulevya
akiwamo mfanyabiashara maarufu Ali Hatibu Haji maarufu Shikuba na wenzake,
Mahakama Kuu inatarajia kusikiliza pingamizi la washtakiwa hao la kukataa kupelekwa
Marekani, Mei 28, mwaka huu.
Watuhumiwa wengine ni Idd Mfuru na Tiko Emmanuel.
Pingamizi hilo linatarajiwa kusikilizwa na Jaji Sawaji wa mahakama hiyo na
washtakiwa watawakilishwa na Wakili Majura Magafu na Hudson Ndusyepo.
Magafu na Ndusypo walifikia hatua ya kukata rufaa baada
ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kutoa uamuzi kuwa wanapinga
uamuzi wa kukubali maombi ya Waziri wa Sheria Katiba ya kuwasafirisha Shikuba
na wenzake kwenda Marekani kujibu tuhuma za kujihusisha na dawa za kulevya.
Hata hivyo, wakati wanasheria hao wanasubiri rufaa yao
ipangiwe tarehe na Jaji wa kusikiliza pingamizi hilo, kuna taarifa kuwa Shikuba
na wenzake wamesafirishwa kwenda Marekani.
Hali hiyo ilisababisha mkanganyiko kutokana na kwamba,
tayari watuhumiwa walipeleka pingamizi Mahakama Kuu na kabla ya kusikilizwa
wakaondolewa nchini, kwa hiyo tarehe hiyo ndiyo itajulikana kama wapo nchini au
la.
“Mei 28 mwaka huu ndiyo Mahakama itatueleza kama wateja
wetu wapo nchini au la kwa sababu hata sisi tumesikia wateja wetu wamesafirishwa
tayari,” alisema Ndusypo akizungumza kwa njia ya simu na JAMBO LEO
Awali, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu,
Cyprian Mkeha alikubali washtakiwa hao wasafirishwe kwenda Marekani na pia
aliamuru wafanyabiashara hao wakae rumande hadi Waziri wa Sheria na Katiba
atakapopata kibali cha kuwasafirisha.
Uamuzi huo ulitolewa baada ya Wakili wa Serikali Mkuu,
Edwin Kakolaki kuwasilisha maombi hayo.
Wakati maombi hayo yanasikilizwa Kakolaki alidai kuwa
maombi hayo yameambatanishwa na hati ya kiapo cha Wakili wa Serikali Msaidizi
wa Marekani Texas, Richard Magnes ambacho kilithibitishwa mbele ya Jaji Nancy
Johnson.
Kiapo hicho kinaeleza watuhumiwa walivyoshiriki katika mashtaka hayo na katika ushahidi inaelezwa kuna mtu alikuwa
amepandikizwa kuchunguza namna wanavyoingiza dawa za kulevya Marekani.
0 comments:
Post a Comment