Profesa Ibrahim Khamis Juma |
KAIMU Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof.
Ibrahim Khamis Juma, amesifu kasi ya uondoshaji wa mashauri katika ngazi za
mahakama za mwanzo na wilaya.
Alisema hayo jana katika ukumbi wa
mikutano ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara alipokuwa akizungumza na watumishi
wa mahakama mkoani
Alikuwa katika ziara yake ya kwanza
tangu kuteuliwa kwenye nafsi hiyo Januari, mwaka huu.
Prof. Juma alisema kuwa wananchi wengi
bado wana imani na mahakama hizo, hivyo idadi kubwa ya mashauri yameendelea
kufunguliwa katika mahakama nchini hususani za chini
“Takwimu tulizo nazo kwa mwaka jana,
asilimia 71 ya mashauri yalifunguliwa katika Mahakama za Mwanzo, 14 Mahakama ya
Wilaya, asilimia saba, mahakama za hakimu mkaz, asilimia tano Mahakama Kuu na
asilimia 0.5 mahakama za rufani,” alieleza.
Aliendelea kusema kuwa takwimu hizo
zinaonesha dhahiri kuwa wananchi bado wana imani kubwa na mahakama nchini na
hivyo kuwataka mahakimu na watumishi wote wa mahakama kuongeza bidii katika
kuwatumikia wananchi.
Mbali na pongezi hizo, aliwataka
watumishi hao kufanya kazi kwa kuzingatia mpango mkakati wa mahakama.
“Wengi wenu mnafahamu kwa sasa, mahakama
ipo katika utekelezaji wa mpango mkakati wake wa miaka mitano, wenye lengo la
kuboresha maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma ya utoaji haki
nchini pamoja na kurejesha imani ya wananchi kwa chombo chao,” alisema.
Aliwataka kujikita katika Matumizi ya
TEHAMA ili kurahisisha utendaji kazi huku akitilia mkazo kwa Watumishi pia
kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya kazi.
Awali, akisoma hotuba yake mbele ya Jaji
Mkuu, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara, Mhe. Devotha
Kamuzora alisema kuwa Mahakama katika mkoa huo zimekuwa zikifanya kazi ya
uondoshaji mashauri kwa jitihada ili kuhakikisha kuwa inaondokana na mlundikano
wa kesi.
“Kwa upande wetu, mahakama kanda ya
Manyara tumejiwekea mkakati wa kuhakikisha kuwa kesi yoyote inayoletwa katika
mahakama ya mwanzo, wilaya isizidi miezi mitatu mpaka kukamilishwa kwake na
hili tunalisimamia kuhakikisha tunaondokana na mlundikano wa mashauri katika
Mahakama zetu,” alisema Kamuzora.
Ziara ya Kaimu Jaji Mkuu imelenga katika
kuangalia utendaji kazi wa Mahakama hizo, mafanikio na changamoto
wanazokabiliana nazo na hatimaye kushughulikia changamoto hizo kwa ustawi wa
Mahakama.
0 comments:
Post a Comment