Joyce Kasiki, Dodoma
Samia Suluhu |
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ameonesha masikitiko kwa
kuongezeka kwa vifo vitokanavyo na uzazi kutoka 432 hadi 556 kwa kila vizazi
hai 100,000.
Akizungumza mjini Dodoma jana katika maadhimisho ya siku
ya Mkunga duniani inayofanyika Mei tano ya kila mwaka, Samia alisema
Serikali imerudi nyuma kwenye utekelezaji wa lengo namba nne la millenia la
kupunguza vifo hivyo.
Alisema vifo vingi vitokanavyo na uzazi, vinaweza
kuepukika iwapo kasoro zilizopo zikiwemo za ukosefu wa vifaa tiba na utaalam wa
wakunga zitarekebishwa.
“Ni jambo la kusikitisha kuona tunarudi nyuma kwenye
suala zima la vifo vitokanavyo na uzazi, Tanzania ilikwishapiga hatua katika
jitihada ya kutimiza lengo namba nne la Millennia.
“Hairidhishi kuona wakati dunia imeanza utekelezaji wa
ajenda ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030, Tanzania inapoteza akinamama 556
kutokana na vifo kwa kila vizazi hai 100,000,"alisema Samia
Hata hivyo Serikali kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ilieleza
kufanya jitihada za kufikia malengo ya 2016- 2020 kwa kupunguza idadi vifo hadi
kufikia 292, huku akisema hata idadi hiyo bado ni kubwa katika suala zima la
vifo hususan vitokanavyo na uzazi.
Moja ya hatua hizo ni pamoja na kuongeza Bajeti ya wizara
kutoka bilioni 796 mwaka 2016/17 hadi trilioni 1.1 kwa mwaka
2017/2018 ambapo Sh bilioni 30 zimeelekezwa kwenye sekta ya mama na mtoto.
Katika fedha hizo za mama na mtoto, Sh bilioni 14
zitagharamia uzazi wa mpango na dawa za uzazi salama, Sh bilioni saba,
ununuzi wa mashine za ultra sound kwa vituo 65 huku Sh bilioni 6 zikitengwa kwa
ajili benki ya damu, kwa kuwa ukosefu wa damu ni moja ya matatizo makubwa
katika uzazi ambapo chupa 1,000 zinahitajika kwa mwezi.
“Ni matumaini yetu kuwa Bajeti ya mwaka 2017/18
iliyoidhinishwa na Bunge itasaidia kusukuma suala la uzazi salama na afya ya
mama na mtoto,” alisema.
Maadhimisho hayo yalianza siku tatu zilizopita ambapo
kati wanawake zaidi ya 100 waliopata nafasi ya kuchunguzwa afya zao, watatu
walibainika kuwa na saratani ya shingo ya kizazi na sita walikuwa na dalili za awali.
Awali Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu aliwataka wakunga kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia maadili ili
kuokoa maisha ya mama na mtoto.
0 comments:
Post a Comment