Joyce Kasiki, Dodoma
BUNGE limeelezwa
kwamba hadi sasa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) inazidai taasisi mbalimbali
za Serikali zikiwamo wizara zaidi ya Sh.bilioni 11.
Kufuatia madeni
hayo, taasisi hizo zimetakiwa kulipa madeni hayo haraka kabla serikali
haijachukua hatua styahiki dhidi yao.
Naibu Waziri wa
Maji na Umwagiliaji Isack Kamwelwe alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali
la Mbunge wa Arusha Magharibi Gibson Ole Maiseyeki (Chadema).
Maiseyeki
alihoji serikali kama haioni sasa umefika wakati wa kuifuta Temesa na Mamlaka
ya udhibiti wa ununuzi wa umma(PPRA) au kuvibadilishia utaratibu wake wa
kufanya kazi ili viweze kuwa na tija kwa Taifa.
Akijibu swali
hilo, Kamwelwe alisema changamoto kubwa inayoikabili Temesa ni madeni makubwa
ambayo Wakala unadai Wizara, Taasisi za serikali na Halmashauri.
Alisema
kuchelewa kulipwa madeni hayo kunaipunguzia Temesa uwezo wa kutoa huduma.
“Serikali
itaendelea kusimamia Temesa ili kuhakikisha kuwa kuna usimamizi wa karibu wa
ubora wa matengenezo ya magari na karakana zake zinatumia vipuri halisi katika matengenezo
ya magari,”alisema
Aidha alisema
serikali itahakikisha kuwa huduma za Temesa zinaboreshwa na kutolewa kwa
ufanisi bila urasimu wowote kwa kufuata mkataba wa huduma kwa wateja na
mwongozo wa matengenezo ya magari ya serikali.
Alibainisha
kwasasa Temesa ina jumla ya wahandisi 78 na mafundi 344.
Kuhusu PPRA,
Naibu Waziri huyo alizishauri Wizara, Taasisi na Halmashauri nchini kuendelea
kuzingatia sheria ya ununuzi wa umma ya mwaka 2011 pamoja na kanuni zake na
kuendelea kutumia huduma za Temesa.
0 comments:
Post a Comment