Stella Kessy
Askofu Josephat Gwajima |
ASKOFU wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima,
jana alitumia Ibada ya Jumapili kuvunja utabiri wa Nabii Shepherd Bushiri aliyedai kuwa uchumi wa
Tanzania utaporomoka na kutabiri kuwa kati ya Rais John Magufuli na Waziri Mkuu
wa zamani, Edward Lowassa, mmoja wao atafariki dunia.
Katika ibada iliyofanyika jana katika kanisa lake
lililopo Ubungo jijini Dar es Salaam, Gwajima alisema utabiri na madai ya
mchungaji huyo wa nchi ya Malawi yameshindwa rasmi na kwamba Tanzania
haitaporomoka kiuchumi.
"Hata Rais Magufuli na Lowassa hawatakufa, nao
wataishi kwa agizo la Mungu," alisema Gwajima.
Nabii Bushiri katika mahubiri yake ya hivi karibuni
amekuwa akitabiri masuala mbalimbali duniani, ikiwemo vifo vya viongozi hao
jambo ambalo kwa nyakati tofauti limezua taharuki miongoni mwa Watanzania.
"Nashangazwa sana na manabii wanaotoa unabii kuwa
viongozi watakufa. Wanasahau kuwa
viongozi wamewekwa kwa mpango wa Mungu na kila wafanyalo Mungu anawasimamia.
Leo nimeamua kuvunja kila hila ambazo
zinapangwa kwa viongozi hawa na kunena mabaya ya nchi yetu, "alisema
Gwajima.
Huku akisisitiza uchumi kuimarika, Gwajima alisema hakuna
kifo kitakachotokea labda kama nabii huyo ana mpango wa kuwaua viongozi hao kwa
mkono wake mwenyewe.
"Ni bora aseme kuwa unabii wake umetimia..., nafuta hati ya kifo na kuwaombea waishi
miaka mingi pia wale wanaowaombea kufa ni mawakala wa shetani hivyo hawana
nafasi katika hilo," alisema.
"...kwangu hamna nafasi kabisa, ninazidi kumwomba Mungu ili viongozi wangu waishi na kuimarika zaidi ili
kuweza kufanya mambo makubwa katika nchi ikiwa ni pamoja na kuboresha uchumi.
Wapo wanaosema Tanzania ni maskini, nafuta kauli hizi, nchi yetu ni
tajiri."
Alisema ataendelea kuliombea Taifa na viongozi mbalimbali
bila kujali itikadi zao na kubainisha kuwa lengo lake ni kuona Taifa likisonga
mbele.
"Tanzania ni nchi iliyofanikiwa sana. Imekuwa na
viongozi wazuri na siku moja tutakaa juu ya mlima na kueleza mafaniko ya nchi
yetu," alisema.
Huku akishangazwa na tabia ya nabii huyo kupenda kutabiri
mambo ya Tanzania na kuacha ya nchini kwake, Askofu Gwajima alisema,
"sijasema kuwa si nabii, huenda amekodishwa kutoa unabii kwa nchi yetu na
mimi ili kuliondoa hilo ninawafunika viongozi wetu kwa damu ya Yesu."
Mbali na kuwaombea viongozi na Taifa, pia aliliombea
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kutekeleza majukumu yake
kikamilifu.
0 comments:
Post a Comment