Grace Gurisha
Do Many Hong |
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemhukumu,
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Halotel Viettel Tanzania Ltd, Do Many Hong na
wenzake saba kulipa zaidi ya Sh milioni 700, baada ya washitakiwa hao kukiri
kutenda makosa saba kinyume na taratibu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA).
Pia imewaamuru washitakiwa hao kuirudishia TCRA, Sh
milioni 459, baada ya kukiri kuisababishia hasara hiyo, kutokana na kufanya
biashara hiyo ikiwamo kufunga vifaa vya mawasiliano bila kufuata utaratibu.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Wilbard
Mashauri, baada ya washitakiwa hao kukiri kutenda makosa hayo, ambapo alisema
watatakiwa kulipa Sh milioni tano kwa kila kosa na pia vitu vya mawasiliano
ambavyo walikutwa navyo vichukuliwe na Serikali.
“Kila mshitakiwa atatakiwa kulipa Sh milioni tano kwa
kila kosa na ile hasara mliyoisababishia Serikali muilipe TCRA na vile vitu
walivyokutwa navyo vichukuliwe na Serikali,” alisema Mashauri.
Baada ya kutoa hukumu hiyo, aliwaeleza kuwa wanaweza
kukata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania, kama hawajaridhika na adhabu aliyoitoa.
Kabla ya hukumu hiyo, Wakili wa Serikali, Jehovanes
Zacharia aliwaondolea mashitaka matatu washitakiwa hao, ambayo ni kula njama,
kuwasilisha nyaraka za uongo na kughushi na kubaki saba, kwa sababu awali
walikuwa wakituhumiwa kwa makosa 10.
Baada ya hapo, washitakiwa walikiri kutengeneza mfumo wa kutumia huduma za mtandao kwa lengo
la kukwepa kodi na makosa mengine sita. Walisomewa maelezo yao ya awali kuhusu tuhuma
zao wakakiri tena, wakatiwa hatiani.
Hata hivyo, Zacharia alidai kuwa hawana kumbukumbu kama
washitakiwa hao walitenda makosa ya jina, kwa hiyo Mahakama iwape adhabu stahiki.
Mbali na Hong, wengine ni Dilshad Ahmed (36), Rohail
Yaqoob(47), Khalid Mahmood (59), Ashfaq Ahmad (38), Muhamad Aneess(48), Imtiaz
Ammar (33) wote raia wa Pakistani na Ramesh Kandasamy (36) wa Sri-Lanka.
Ilidaiwa kuwa Novemba 20, mwaka jana washitakiwa waliingiza
vifaa vya elektroniki bila leseni na katika siku isiyofahamika Novemba mwaka
jana, walisimika vifaa hivyo ikiwamo sim box yenye namba ya siri
1152000.8.n.t.n na kompyuta mpakato mbili aina ya Dell bila kibali cha TCRA.
Katika kipindi hicho, washitakiwa hao waliunganisha vifaa
hivyo na huduma za mitandao kwa lengo la kupokea na kusambaza mawasiliano bila
kuthibitishwa na TCRA.
Hong ilithibitishwa kuwa kati ya Novemba mwaka jana na
Februari maeneo ya ofisi za Halotel Victoria Kinondoni, alishindwa kuthibitisha
taarifa iliyotolewa na Unex Company Ltd kwa lengo la kusajili simu 1,000.
0 comments:
Post a Comment