Lipumba adai Jecha bora kuliko Maalim


*Asema kiini cha mgogoro ni mfumo wa serikali
*Aendelea kumtambua kama Katibu Mkuu halali

Celina Mathew
Profesa Ibrahim Lipumba
MWENYEKITI wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, amesema anavyoona Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha ni bora kuliko Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharrif Hamad.

Wawili hao wamekuwa na mvutano na kutupiana vijembe kwa muda sasa baada ya Lipumba aliyejitoa CUF Agosti mwaka juzi kuamua kurejea ndani ya chama hicho mwaka jana na kuzua mgogoro.

Kutokana na mgogoro huo, CUF imegawanyika mapande mawili, moja la Lipumba ambaye pia anatambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini na lingine la Maalim Seif.

Lakini jana Profesa Lipumba alitaja kiini kingine cha mgogoro wake na Maalim Seif ndani ya CUF kuwa ni Mchakato wa Katiba mpya mwaka 2013 wakati wa Bunge la Katiba ambapo Maalim Seif alikuwa akipigania kuwepo Muungano wa Mkataba huku Lipumba na msimamo wa chama ukiwa ni Serikali tatu.

Jecha alifuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar mwaka juzi, kabla ya kurudiwa Machi 20 mwaka jana na Dk Ali Mohammed Shein wa CCM kushinda, huku CUF ikisusia uchaguzi huo.

Lipumba alisema hayo jana alipotakiwa kueleza kiini na sababu zinazoendeleza mgogoro ndani ya CUF, uvamizi wa mkutano, kuvamia ofisi za chama Buguruni, kushiriki kwenye mchakato wa kumpokea Edward Lowassa ndani ya Ukawa na msimamo wake wa kuomba kujiuzulu.

Akizungumza kupitia kipindi cha 360 kinachorushwa na kituo cha Clouds Media, Lipumba alionekana kumrushia mpira Maalim Seif kuwa ndiye chanzo cha mgogoro na kwamba hana ushirikiano.

“Bora ya Jecha Salum Jecha aliyefuta uchaguzi Zanzibar kuliko Maalim Seif aliyetangaza matokeo kabla ya uchaguzi kufanyika,” alisema na kuongeza:

“Mimi sijakataa kufanya kazi na Maalim, tatizo lake ni kuwa kila nikimwita ofisini nimpangie majukumu anagoma kuja, hivyo hali hiyo imesababisha mgogoro uzidi kuwepo ndani ya chama na hakuna ushirikiano wowote.”

Alisema kwa kiasi kikubwa, Maalim Seif amekuwa akivunja Katiba ya chama na kwamba angeiheshimu matatizo kama hayo yasingeweza kujitokeza.

“Maalim anajiona Sultani wa chama, maana hata wakati naandika barua ya kujiuzulu, baadaye nilishauriwa na wananchi nikaona bora nitengue barua yangu, kwa kuwa mimi sikuwa wa kwanza,” alisema.

Alisema Katiba haijakataza mtu aliyejiuzulu kutengua uamuzi wake, kwa kuwa Nassoro Mazrui alipogombana na Maalim Seif alijiuzulu, lakini baadaye aliamua kurudi.

Katiba inasema mtu akijiuzulu kama mchakato haujakamilika wa wajumbe wa Kamati Kuu, pande mbili za Zanzibar na Tanzania Bara wapige kura kila upande upate theluthi mbili ndipo mtu anakuwa amejiuzulu, jambo ambalo halikufanyika.

Alisema baada ya kuandika barua ya kujiuzulu kwa Maalim Seif, jambo la kushangaza aliitisha Mkutano Mkuu ili kumjadili Lipumba na kupiga kura, jambo ambalo baadaye lilivurugika na kuamua kutangazwa matokeo ya kura wakati uchaguzi haukufanyika.

Kiini

Akizungumzia chanzo cha migogoro ndani ya chama hicho, alisema ilianza mwaka 2013 kwenye Bunge la Katiba wakati Maalim alipotaka kuwepo Muungano wa Mkataba jambo ambalo Lipumba alilipinga.

“Maalim alikuwa na lengo la kuvunja Muungano, hivyo nilikataa suala hilo kwa kuwa Muungano uliopo ni wa serikali tatu na dhamira yetu ni kuwapo na unaoendana na wa Jaji Nyalali (marehemu Francis) ambao kwa sasa ni wa Jaji Mkuu mstaafu Joseph Warioba hivyo kana ningekubali uliopo ungevunjwa,” alisema.

Januari 14, 2013 Maalim Seif alipokuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alitoa mapendekezo yake kwa Tume ya Maoni ya Katiba, kuwa kutokana na uzoefu wake wa miaka 49 wa Muungano wa Katiba kati ya Zanzibar na Tanganyika, alipendekeza nchi hizo ziingie kwenye mfumo wa Shirikisho kupitia Muungano wa Mkataba.

Alisema chini ya Muungano huo wa mkataba kuwe na serikali mbili ambapo Jamhuri ya Tanganyika itakuwa na serikali yake na Zanzibar itakuwa na ya kwake ambapo zote mbili zitakuwa na mamlaka kamili kitaifa na kimataifa.

“Kisha Serikali hizo mbili zitaingia mkataba wa ushirikiano baina yao ambao unaweza ukapewa jina la ‘Tanzanian Union Treaty’. Yale maeneo yatakayokubaliwa kuwa chini ya ushirikiano wa nchi mbili huru yatasimamiwa na Kamisheni ya Muungano, kama ilivyo kwa Kamisheni ya Ulaya au jina lingine lolote litakalokubaliwa na nchi mbili hizo,” alisema kupitia hotuba hiyo.

Lowassa

Akizungumzia moja ya sababu za migogoro ndani ya chama hicho, Lipumba alisema wakati mgombea urais kupitia ukawa, Lowassa alipoteuliwa Maalim hakumhusisha kwenye vikao, bali alimletea taarifa tu.

Alisema Maalim alimwambia kwa kuwa CUF haina fedha za kujiendesha, ni vema wakamkubali Lowassa asimame kama mgombea wa Ukawa.

Sumaye

Profesa Lipumba alionekana kumshangaa Maalim Seif kwa kueleza kuwa amemsamehe Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye wakati kipindi cha uongozi wake, walitangaza kufanya maandamano ya amani lakini cha kushangaza wanachama wa chama hicho zaidi ya 60 walipoteza maisha.

“Tuliiomba Serikali kufanya maandamano ya amani baada ya uchaguzi wa Zanzibar ili urejee kipindi hicho, ambacho Sumaye ndiye alikuwa Waziri Mkuu kwenye Serikali iliyokuwa madarakani, lakini cha kushangaza tulipigwa na mimi nikavunjwa mkono, hivyo namshangaa Maalim anaposema amemsamehe nahisi ana matatizo,” alisema.

Alisema kwa kiasi kikubwa wao kama viongozi walijisaliti kwa kujiunga na Ukawa huku wote wakijinadi kuwa watapambana na ufisadi kisha wakachukua uamuzi wa kumchukua Lowassa awe mgombea wakati ni CCM.

“Tulimpokea Lowassa tukasema masuala ya kupambana na rushwa ni ya wote, si mmoja bali kujenga mfumo lakini sikusema kama nitamnadi, licha ya kwamba nilikwenda kwake nikazungumza naye kuhusu yeye kuhamia nilimshauri hilo suala wazungumze na vyama vyote vinavyounda Ukawa si Chadema pekee.

“Nilikwenda nikazungumza naye kwamba hata ACT- Wazalendo washirikishwe kwenye mchakato, badala yake Maalim alikutana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kwa siri na kufanya uamuzi,” alisema.

Ikulu

Akifafanua alichokwenda kufanya Ikulu baada ya Rais John Magufuli kuapishwa, alisema aliitwa Ikulu kwenda kuzungumza naye kuhusu suala la uchaguzi Zanzibar.

“Niliitwa Ikulu na Rais Magufuli tukazungumza kuhusu suala la uchaguzi wa Zanzibar, akaniambia kuwa tutakavyokubaliana yeye ataunga mkono nikaenda kumweleza Maalim ambaye naye alipata fursa ya kuonana naye,” alisema.

Ofisi

Akitoa ufafanuzi kuhusu yeye kuvamia ofisi za chama Buguruni, alisema hakuvunja bali hatua hiyo ilitokana na utambuzi wa Msajili kwake kama Mwenyekiti wa Chama.

“Sikuvunja ofisi bali nilikwenda pale na walinzi wa chama, Blueguards, tukagonga lakini mlango haukufunguliwa, kwa kuwa ilikuwa imewekwa kampuni binafsi ya ulinzi jambo ambalo ni kinyume na Katiba,” alisema.

Alisema kwa kuwa lango lilifungwa, walinzi wa chama ambao Maalim Seif juzi aliwaita maharamia licha ya kuwa ndiye aliwapa vitambulisho walipanda uzio na kufungua kwa nguvu. 

Alisema baada ya kuingia walikaribisha wanachama upya ili kuweka mikakati ya kujenga chama yeye akizunguka wilaya na mikoa yote na kufanya mkutano na viongozi.

Hata hivyo, aliweka wazi kuwa anamtambua Maalim kama Katibu Mkuu hivyo “hakuna CUF yangu wala yake bali ni ya wanachama”.

Uvamizi

Alipoulizwa anahusikaje na uvamizi wa mkutano wa hivi karibuni Mabibo, alisema kwa kiasi kikubwa hausiki na suala hilo kwa kuwa hawana utaratibu wa kwenda kuvamia mikutano ya upande wa pili.

Aliongeza kuwa kipindi cha nyuma wakati wa mfumo wa vyama vingi aliwahi kuwa mshauri wa mambo ya kiuchumi wa Rais Alhaji Ali Hassan Mwinyi lakini baadaye alihamia CUF baada ya kuombwa  na Hamad Rashid Mohamed kugombea urais kupitia CUF mwaka 1995.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo