Grace Gurisha
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam imewaacha
huru wabunge watatu wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na madiwani wawili waliokuwa
wakikabiliwa na kesi ya kumjeruhi Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Theresa Mmbando.
Wabunge hao ni Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, Mbunge wa
Ukonga, Mwita Waitara huku madiwani ni wa kata ya Kimanga, Manase Njema, wa
Saranga, Ephraim Kinyafu na kada wa chama hicho, Rafii Juma.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma
Shaidi wa Mahakama hiyo, baada ya kuwaona washitakiwa hao hawana kesi ya
kujibu.
Alisema ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa
mashitaka ulishindwa kuthibisha bila kuacha shaka lolote.
Pia alisema hata mlalamikaji Mmbando hakumbuki ni nani
alimjeruhi siku ya tukio hilo, ambapo katika ushahidi wake alieleza jinsi washitakiwa
walivyojishughulisha na nyaraka na si kumjeruhi.
Kuhusu suala la Mmbando kudai alishikwa matiti wakati wa
mvutano na washitakiwa hao, Hakimu Shaidi alisema alishikwa matiti, lakini hajui
alishikwa na nani. Hivyo aliwaacha huru washitakiwa wote kwani hawakuwa na kesi
ya kujibu.
Kesi hiyo ilikuwa ikiendeshwa na Wakili wa Serikali, Florentina
Sumawe ambaye aliita mashahidi watatu. Machi 14, alifunga ushahidi wao na
Hakimu Shaidi kuupitia na kufikia uamuzi huo.
Washitakiwa hao wanadaiwa kuwa Februari 27 mwaka jana
katika ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam, walimjeruhi Theresia. Washitakiwa
wote walikuwa nje kwa dhamana.
Mmbando wakati akitoa ushahidi wake alieleza jinsi
alivyovamiwa, kujeruhiwa na kupokonywa jalada lililokuwa na ajenda na mwongozo
wa uchaguzi wa Meya na Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, uliopaswa kufanyika
Februari 27 mwaka jana.
Alidai kuwa siku hiyo alipewa jukumu la kusimamia uchaguzi
huo wa Meya na Naibu Meya ambao ulipaswa kufanyika saa 4 asubuhi kwenye ukumbi huo.
Katibu Tawala alikuwa Mwenyekiti wa uchaguzi huo, wajumbe
wote walifika, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Salehe Yohana ambaye alikuwa
Katibu alifungua uchaguzi huo kwa sababu akidi ya wajumbe ilitimia.
Baada ya kikao kufunguliwa na Katibu huyo, Salehe alisema
uchaguzi huo hautafanyika kwa sababu alipokea zuio la Mahakama dhidi ya
uchaguzi huo na akawaarifu wajumbe.
Wajumbe wa CCM walitoka nje lakini wa vyama vingine
wakiwamo wa Ukawa walimvamia wakimshinikiza aendeshe uchaguzi huo.
0 comments:
Post a Comment