Abraham Ntambara
KAMPUNI ya Reli Tanzania (TRL), imesimamisha
kwa muda wa siku 14 huduma ya usafiri wa treni kutoka Dar es Salaam hadi
Morogoro, ili kupisha marekebisho ya miundombinu iliyoharibiwa na mvua.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Masoko wa TRL,
Shaban Kiko alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari Dar es
Salaam kuhusu daraja la reli la Ruvu kutitia upande mmoja.
Kutokakana na hali hiyo, alisema abiria
257 waliotakiwa kusafiri jana kutoka Dar es Salaam, watasafirishwa leo kwa mabasi
na kampuni hiyo hadi Morogoro kili kuendelea na usafiri wa treni.
“Uamuzi huu umechukuliwa kutokana na
kipande cha reli kati ya Dar es Salaam na Ruvu kuwa haipitiki,” alisema Kiko.
Alisema mamlaka husika zinafanyia kazi
ukarabati wa daraja hilo ili njia ya reli kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro
ifunguliwe ndani ya muda mfupi iwezekanavyo.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka abiria wanaosafiri
leo kufika kituo kikuu cha reli Dar es Salaam kabla ya saa moja asubuhi, ili wasafirishwe
kwa mabasi maalumu yaliyokodiwa na TRL hadi Morogoro ambako watapanda treni
kwenda Bara, itakayoondoka saa moja usiku.
Akizungumzia wafanyabiashara
wasafirishao shehena kwenda Bara, aliwataka kuwasiliana na Idara ya Masoko ya
TRL ili kupewa utaratibu wa jinsi ya kusafirisha mizigo yao hadi Morogoro
ambako itapakiwa kwenye treni kwenda Bara.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Bodi ya
TRL, Profesa John Kondoro na wajumbe wengine wa Bodi hiyo jana asubuhi
walitembelea eneo la daraja hilo kufanya tathmini ili kuruhusu maandalizi ya
ukarabati kuendelea.
0 comments:
Post a Comment