Taifa linahitaji msaada wa saikolojia



Mashaka Mgeta

TUKIO la kushambuliwa kwa majengo pacha ya Kituo cha Kimataifa cha Biashara (WTO), Septemba 11, 2001 jijini New York, Marekani, liliibua taharuki na kuchanganyikiwa kwa watu nchini humo.

Vyombo vya habari viliripoti tukio hilo katika mtazamo na kuandika ama kutangazwa kwa mwonekano tofauti. Mwandishi wa habari mkongwe wa gazeti la New Yorker, Lilian Ross, alikuwa miongoni mwa waandishi walioshiriki kukusanya taarifa na kuandika habari inayohusiana na tukio hilo.

Kupitia kitabu chake cha Reporting Back, Notes On Journalism, Ross anaeleza jinsi Mhariri wake alivyomuelekeza ajikite katika athari za mlipuko huo wa kigaidi kwa watoto. Waandishi wenzake walielekezwa katika maeneo tofauti ili kupata wigo mpana wa kuandika kuhusu tukio hilo.

Ross alikwenda kwenye moja ya shule za msingi zilizopo ukanda wa juu wa mashariki jijini humo, alipokuta taratibu za kuwaruhusu wanafunzi kurejea nyumbani zikiwa zimekamilika, hivyo wazazi walisubiriwa ili wakabidhiwe watoto wao.

“Tuliamua tusiwe watu wa kwanza kuwajulisha watoto (wanafunzi) kuhusu kulipuliwa kwa WTO, tulitaka wazazi wao waamue nini na namna gani ya kuwaambia kuhusu tukio hilo,” Ross alimkaririwa Mkuu wa shule hiyo, Dan Fiegelson akisema.

Kwa mujibu wa hekaya ya Ross kuhusu tuko hilo, Serikali ya Marekani iliamuru kufungwa kwa shule hizo. Siku iliyofuata Fiegelson alikuwa miongoni mwa walimu wakuu 40 walioitwa ofisi ya wilaya, wakapata mafunzo ya saikolojia kutoka kwa wanataaluma wa tasnia hiyo kutoka Chuo Kikuu cha New York.

Lengo la mafunzo hayo ilikuwa kuwajengea uwezo walimu wakuu hao ya namna bora ya kuzungumza na wanafunzi (watoto) kuhusu kulipuliwa kwa WTO pindi watakaporejea shuleni.

“Tatizo langu likuwa ni namna ya kumfafanua watoto wa miaka sita walioshuhudia kupitia runinga, watu wakiruka madirisahani….” Fielgeson akakaririwa akisema.

Mkuu huyo wa shule aliamua kutumia mfumo wa kuzungumza na wanafunzi wa kila darasa, ili kuwahakikishia usalama pindi waliporejea shuleni.

“Niliamua kuwafikia darasani ili niongee nayo uso kwa uso katika kuwahakikishia usalama wao, na kuwataka wanafunzi wakubwa kuwa wema kwa wadogo zao pindi wanapojadiliana kuhusu shambulizi hilo,” akasema.

Shule ilipofunguliwa, Fielgelson alikutana na walimu wenzake saa mbili kabla ya kuwasili kwa wanafunzi, akawaambia, “tunahitajika kuwasaidia wanafunzi waamini kwamba kuna usalama, tutawaambia, shule bado ipo hapa, masomo yataanza saa mbili zijazo lakini kila kitu kipo salama.”

Wanafunzi waliporejea, Fiegelson alianza kuzungumza na wanafunzi wa darasa la tano ambalo ndilo la juu, akawaambia.

“Ninawahakikishia kila mmoja wetu yupo salama, watoto wa madarasa ya chini wanawaangalieni ninyi, huu si wakati wa kuwafanya mizaha ama kuwaogopesha, tunawahitaji kuwa wasaidizi wao. Si wakati wa kuchukiana bali kusaidiana kila mmoja.”

Hiyo ni sehemu ya hekaya ya moja ya matukio yaliyohusiana na kulipuliwa kwa majengo pacha ya WTO, takribani miaka 16 iliyopita, msingi wake ukiwa katika hitaji la msaada wa kisaikolojia kwa kadhia mbalimbali zinazowakabili raia wakiwamo Watanzania.

Nimeandika makala haya kutokana na ajali iliyotokea Mei 6, mwaka huu wilayani Karatu na kusababisha vifo vya wanafunzi 32, walimu wawili na dereva mmoja wa Shule ya Msingi Lucky Vicent ya jijini Arusha.

Yapo majanga mengi yaliyowahi kutokea nchini na kuwaathiri watoto kisaikolojia na yapo mengine yanayoendelea kutokea kama mafuriko, mashambulizi ya silaha yanayosababisha mauaji, japo kwa uchache.

Lakini kubwa ‘lililoliliza taifa’ kiasi cha kugusa hisia za familia ya Mwinjilisti Billy Grahm iliyotoa ndege aina yaDC 8 kupitia Shirika la Samaritan Purse nchini Marekani kuwasafirisha watoto watatu walionusurika katika ajali hiyo, Saida Awadhi (11), Doreen Mshana (13) na Wilson Tarimo.

Kama ilivyokuwa baada ya kulipuliwa kwa jengo la WTO, ‘ajali ya Karatu’ ilisababisha kufungwa kwa muda kwa shule ya Lucky Vicent na kutakiwa kufunguliwa kwa siku saba, lakini taarifa za uongozi wake zikaeleza kuchelewa kurejea kwa wanafunzi.

Si nia yangu kuelezea ukweli kuhusu kuwapo ama kutokuwapo kwa msaada wa kisaikolojia kwa walimu na wanafunzi wa shule hiyo pale ratiba ya masomo itakaporejea baada ya ajali hiyo.

Lakini jambo la msingi hapa ni kwa Taifa kujitafakari, ni kwa namna gani nchi inajielekeza katika kutambua, kuanzisha na kutanua huduma za msaada wa kisaikolojia pindi majanga yanapowakabili watu?

Kwa mfano, kama walimu na wanafunzi wa Shule ya Lucky watakuwa wamepata msaada huo litakuwa jambo jema, tena jema sana. Isipokuwa kama litakuwa jambo lililozoeleka kwa asasi za kijamii kama shule hiyo kukosa ushauri na msaada wa kisaikolojia, hali ya wadau wake hasa walimu na wanafunzi haitakuwa nzuri.

Fikiria wanafunzi walioondokewa na marafiki, ndugu na jamaa waliozoea kuwaona, wakishirikiana katika kazi za nje ya darasa na wakati mwingine wakiwategemea kwa kuwaelekeza, hatawaona tena.

Kila watakapopita mbele ya darasa la saba lililotumiwa na wanafunzi waliofariki, ama kuyaona magari ya wanafunzi yakiingia, kutoka ama kuegeshwa shuleni hapo, kumbukumbu za wenzao waliotangulia mbele za haki itawarejea. Hawatakuwa salama kisaikolojia.

Ni vizuri kulitafakari tuko hilo pia kwa walimu waliokuwa wakiwafundisha wanafunzi waliofariki. Wale waliokuwa mithili ya watoto wa familia moja, wakijiwajibisha katika masomo, wakitaniana, wakipeana taarifa na kuzielezea ndoto za maisha yao ya baadaye, sasa hawatawaona tena kutoka na kufa ghafla.

Katikati ya hali hiyo, ni vizuri Taifa litafakari namna bora ya kuhusisha hitaji la msaada wa kisaikolojia kwa watu wake, kama ilivyo kwa huduma nyingine za jamii ikiwamo sheria, afya nakadhalika.

Mtu anapoathirika kisaikolojia anakuwa mfano wa mgonjwa mahututi aliyepoteza kumbukumbu na uwezo wa kufikiri. Kwa maana saikolojia inayotokana na neno la kiyunani-‘psyche’ lenye maana ya nafsi ama roho.

Hivyo pamoja na tafsiri nyinginezo, saikolojia inabaki kuwa ni sayansi ya kuchunguza ama kujifunza jinsi nafsi ama roho inavyofanya kazi. Kwa maelezo mengine, saikolojia ni elimu ya kisayanzi kujua namna binadamu na wanyama wanavyofanya mambo fulani.

Kwa vile saikolojia inahusu nafsi, pale (nafsi) zinapoathirika hasa kwa asili, kutokana na majanga kama ajali, mashambulizi, vifo, kuyumba kwa hali ya uchumi hasa katika ngazi ya familia nakadhalika, ni vema kukawapo huduma ya msaada wa kisaokolojia.

Ndio maana nilipolitafakari tukio la ajali na vifo vya wanafunzi wa Lucky Vicent, kisha kukamatwa, kuwekwa ndani na kufunguliwa mashtaka kwa wakuu wa shule hiyo, niliona na bado ninaliona hitaji la msaada huo shuleni hapo, ili kurejesha mambo kuwa mazuri zaidi.

Hitaji hilo linapaswa kupatikana ili walimu na wanafunzi watambue, wakubali ndani ya dhamira zao kwamba tukio hilo limepita, si lenye kujirudia mara kwa mara na kwamba kwa umoja wao, wapo salama, wanachopaswa kushiriki ni kuendelea na ratiba zao.

Ni vigumu kwa mtu wa kawaida kuiaminisha jamii hiyo kuhusu ukweli huo ili wauelewe, kuukubali na kuuishi. Ndio maana wakawapo wanataaluma wa saikolojia wanaopatikana katika vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu, walisaidie taifa katika hilo.

+255 754 691 540
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo