*Vyumba vya ICU vyakabiliwa na upungufu mkubwa wa wauguzi
*Mkurugenzi
asisitiza maadili, nidhamu ya kazi na tabia njema
Dalila Sharif
HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili
inakabiliwa na upungufu mkubwa wa wauguzi uliosababishwa na kuondolewa kwa
wauguzi 60 waliokutwa na vyeti bandia vya elimu ya sekondari.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo,
Profesa Lawrence Museru alisema jana kuwa hali hiyo imeathiri zaidi vyumba vya
wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU), ambavyo vinahitaji zaidi wauguzi
kwa ajili ya kutoa huduma kwa wagonjwa hao.
Alisema hayo jana wakati wa maadhimisho
ya Siku ya Wauguzi Duniani, na kutaja sakata hilo kuwa miongoni mwa changamoto zinazoikabili
hospitali hiyo.
“Hospitali yetu imepungukiwa na baadhi ya
wauguzi walioondoka wenyewe kwa kuwa na vyeti bandia,” alisema.
Pamoja na upungufu huo, aliwataka
wauguzi wafanye kazi kwa kufuata maadili ya taaluma, kuwa na nidhamu na tabia
njema na kuwaonya wachache wanaochafua
taswira ya uuguzi.
Aliagiza kila muuguzi awe na
kitambulisho cha kazi kwa ajili ya kutoa huduma na kuwataka waheshimu taaluma yao.
“Mnapaswa kutumia lugha nzuri kwa wateja
wetu ambao ni wagonjwa, mtoe maneno yanayostahili ili kutowakwaza maana yanasemwa
kuwa baadhi ya wafanyakazi hawana lugha nzuri,” alisema Profesa Museru.
“Hivyo wauguzi mshiriki kuongeza mapato ya
ndani ambayo yatakayosaidia kulipa baadhi ya madai na kuhusu suala la sare
tunalifanyia kazi ili kila muuguzi apewe,” alisema Museru.
Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga
wa Hospitali hiyo, Agnes Mtawa alisisitiza kuwa wauguzi wote wanatakiwa kuwa na
leseni ya kazi.
Alisema kitambulisho hicho ndicho
kitakachowawezesha kutoa huduma kwa
wagonjwa na atakayekiuka, atakuwa hatarini kukabiliwa na kifungo cha miaka
mitano jela au faini ya Sh milioni tano.
Agnes alisema wauguzi wengi hufanya kazi
bila leseni hali ambayo ni kinyume na sheria ya utoaji huduma kwa wagonjwa.
“Hivyo sheria hii itachukua mkondo wake
kwa kila muuguzi atakayekwenda kinyume, kwa kutokuwa na leseni ya utoaji huduma
kwa wagonjwa,” alisisitiza Agnes.
0 comments:
Post a Comment