Leonce Zimbandu
MTOTO wa miaka mitano amefariki dunia na
watu wengine sita wa familia moja kukimbizwa katika zahanati ya Kivule wakiwa
hoi, wakidaiwa kula mihogo yenye sumu.
Janga hilo lilitokea juzi eneo la
Uthamini, mtaa wa Mbondole, manispaa ya Ilala na kuzua taharuki kwa majirani na
baadhi ya watu waliofika nyumbani kwa Chacha Fyefye kushuhudia.
Mmoja wa mashuhuda hao ambaye ni dereva
wa bodaboda, Daud Mseti, alidai kwamba alipokuwa kituoni alifuatwa na mtu na
kumweleza afuatane naye kumchukua mgonjwa ili kumpeleka hospitali.
Alidai baada ya kufika nyumbani kwa
Chacha, alikuta watoto watatu wamelazwa chini na kuwabeba kwenye pikipiki na
kwenda nao zahanati ya Kivule.
“Tulipofika Kivule, muuguzi wa zamu
alitupokea vizuri na kutoa huduma, baada ya muda mfupi mama na watoto wengine
walifika katika zahanati hiyo wakiwa hawajitambui,” alidai.
Alidai kuwa ingawa vitanda katika
zahanati hiyo vilikuwa vichahche, lakini wagonjwa hao walipokewa na kupewa
huduma na kunusuru afya zao.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbondole, Thomas
Nyanduli alidai kuwa hali hiyo inasikitisha na kutaka wananchi kuchukua hadhari
ya kununua vitu ovyo na kula na kuwataka wananchi kutoa taarifa haraka ili
hatua zichukuliwe wanapopatwa na matatizo kama hayo.
Alidai, Mama Chacha ni mfanyabishara wa
mboga, ambaye husafirisha mboga alfajiri kwenda kuuza maeneo ya Viwege, hivyo
alipomaliza kuuza bidhaa hiyo, alinunua mihogo hiyo bila kujua.
“Hatuwezi kuthibitisha kama ilikuwa ni
sumu ya namna gani, lakini mtoto mmoja amepoteza maisha baada ya kula mihogo
hiyo na wengine wamekimbizwa zahanati na baadaye katika hospitali ya Amana kwa ajili
ya vipimo,” alisema.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala,
Salum Hamduni alisema hana taarifa ya tukio hilo, lakini akaahidi kulifuatilia
kujua ukweli.
“Sina taarifa, nitafute baadaye lakini
kwa sasa sina jibu la moja kwa moja,” alisema.
0 comments:
Post a Comment