Mwandishi Wetu
Godbless Lema |
WAKATI CCM ikidai kuwa Katibu Mkuu wake,
Abdulrahman Kinana, amepewa likizo bila kutaja muda maalumu, Mbunge wa Arusha
Mjini, Godbless Lema (Chadema), amedai bungeni kuwa kuna taarifa kiongozi huyo
amefichwa.
Juzi Katibu wa Halomashauri Kuu (NEC) ya
CCM, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole akiwa mkoani Arusha, alikaririrwa akisema
kuwa Kinana yuko katika mapumziko ya kutazama afya yake.
Lakini wakati Polepole akitoa taarifa
hiyo, bungeni Lema alidai kuwa amesoma taarifa katika mitandao ya kijamii kuhusu
kufichwa kwa Kinana.
Akichangia juzi katika vikao vya Bunge
vinavyoendelea mjini Dodoma, Lema ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani,
alisema kumekuwepo na taarifa nyingi za kufichwa kwa Kinana.
Kutokana na taarifa hizo za mitandao,
Mbunge huyo aliwataka wabunge kuungana na kupaza sauti bila kufumbia macho taarifa
hizo.
Katika hotuba yake hiyo bungeni, Lema
alisema kutokuwepo kwa uhuru wa habari nchini kumechangia watu wengi kuwa waoga
na kushindwa kuhoji juu ya taarifa zinazoibuliwa mitandaoni.
Alitoa mfano kupotea kwa aliyekuwa
Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na kada wa chama hicho, Ben
Saanane kuwa taarifa ya kupotea kwake ilianzia mitandaoni.
“Hata suala la Ben Saanane lilianzia
huko kwenye mitandao, lakini tukakaa kimya kwa uoga, leo yapata miezi sita
tangu kupotea kwake, hili la Kinana kama mkiamua kukaa kimya mimi nitamtetea
kama Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani.
“Kumekuwa hakuna uhuru wa kuongea kila
sehemu, si bungeni, kwenye mitandao ya kijamii wala mitaani. Watu wanaogopa
kuzungumza na kukaa na vitu mioyoni mwao, siku wakichoka wataingia barabarani
bila kuambiwa na Chadema na CUF na hakuna kati yenu atakayesalia,” alisema
Lema.
Alisema si vema Serikali na Bunge kupuuzia
taarifa hizo na kuwataka wabunge wa CCM kuungana naye kupaza sauti, kwani leo
wanaumizwa wao wa upinzani na wakimalizwa watahamia upande wa pili wa chama
tawala.
“Nyie mnashangilia Bunge kutokuoneshwa
moja kwa moja, mikutano ya kisiasa kukatazwa lakini niwaambieni, machafuko ya
Syria yalianza baada ya kijana mmoja wa miaka 16 kupaza sauti yake kuwa Assad anapaswa
kuondoka na tangu hapo nchi hiyo imeingia katika machafuko.
“Tunisia kijana mmoja mdogo ndio
alianzisha maandamano na mpaka leo nchi haijatulia inapita katika kipindi
kigumu, nyie mnaona Chadema inapiga kelele, lakini mnapaswa kutambua kuwa
hakuwezi kuwa na Taifa lenye amani pasipo kuwa na uhuru wa habari,” alisema
Lema.
Wakati Lema akiendelea kuzungumza, Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George
Simbachawene aliomba muongozo kwa Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu.
Alipopewa nafasi, Simbachawene alimtaka
Lema kuthibitisha taarifa zake za kufichwa kwa Kinana na kabla ya kujibiwa, Mnadhimu
Mkuu wa Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alinyanyuka kuomba muongozo na kusema
alichokifanya Lema ni kurejea kile alichokisoma mitandaoni na si vinginevyo.
Kinana hajasikika tangu Rais John
Magufuli alipotangaza Machi 24 mwaka huu kuwa amemtuma kwenye matibabu nchini
India na angerudi baada ya siku 14.
Tangu kutolewa kwa kauli hiyo, hivi
karibuni kulikuwepo taarifa katika mitandao ya kijamii ikielezwa kuwa Kinana
alifichwa huku wengine wakieleza kuwa alionekana nchini Canada.
0 comments:
Post a Comment