Mwandishi Wetu, Dodoma
MAKAMU wa Rais,
Samia Suluhu Hassan, ameagiza miradi yote yenye thamani isiyozidi Sh bilioni 10
wapewe wakandarasi wa ndani akielekeza hilo lifanyike hasa kwa miradi
inayotekelezwa kwa fedha za ndani.
Samia amesema
kwa kufanya hivyo, wakandarasi hao watasaidia kuongeza ajira kwa vijana wa kitanzania
na uwekezaji ndani ya nchi.
Makamu wa Rais
alitoa kauli hiyo mjini hapa
jana wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa mashauriano wa Bodi ya Usajili
wa Wakandarasi wa mwaka huu.
Alisema ni
muhimu kwa wakandarasi hao kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili na sheria na
kumaliza kazi wanazopewa ndani ya muda uliopangwa, kwa kuzingatia ubora wa kazi
na gharama zilizokubalika kwenye mikataba na si vinginevyo.
Makamu wa Rais pia
alionya wakandarasi nchini kuacha kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa, ili
kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wanayopewa.
“Serikali
itaendelea kuwapa kipaumbele wakandarasi wazawa ili wathubutu kujitosa na kumudu
zabuni za ujenzi, kwani kufanya hivyo kutaleta faida zikiwamo fedha
watakazopata na kuziwekeza ndani ya nchi na kutoa ajira za kutosha kwa vijana
wa kitanzania,” alisema na kuongeza:
“Hatuwezi kuwa na Tanzania ya viwanda huku tukinufaisha wakandarasi wa
nje pekee. Ni lazima wakandarasi wa ndani wanufaike pia.”
Kuhusu madeni, aliwahakikishia
wakandarasi hao kuwa Serikali haijawasahau na kwamba bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano iliyopitishwa na Bunge imezingatia kilio chao.
Aliahidi kuwa Serikali
itaendelea kulipa madeni inayodaiwa na wakandarasi ili kujenga uhusiano mzuri na
wakandarasi hao.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa aliwaambia wakandarasi
kwamba wizara yake inaendelea kusimamia sheria na maadili ili kuhakikisha
miradi ya ujenzi inayotekelezwa inakuwa na ubora unaotakiwa.
Hata hivyo,
Profesa Mbarawa alikiri kuwapo baadhi ya wakandarasi wasiotekeleza majukumu yao
ipasavyo hivyo kujenga miradi kwa kiwango cha chini akiwahimiza kufanya kazi kwa
ubora ili waaminiwe na Serikali na kupewa kazi.
Aliahidi wizara kuendelea
kutenga fedha za kuwajengea uwezo ili kutekeleza majukumu yao kwa viwango
vinavyotakiwa.
Msajili wa Bodi
ya Wakandarasi, Rhoben Nkori alisema Bodi yake imeshafuta usajili wa wakandarasi
3,000 kwa kushindwa kutimiza matakwa ya usajili wa wakandarasi ya mwaka 1997 na
kwamba sasa Bodi ina wakandarasi 9,000 nchini.
Alisema katika
kuratibu mwenendo wa kazi za wakandarasi, Bodi hiyo ilikagua miradi 3,813
ambapo kati yao 2,714 sawa na asilimia 71.2 haikuwa na kasoro na mingine
ilikuwa na kasoro ikiwamo miradi hiyo kutofanywa na wakandarasi waliosajiliwa
na kutozingatia usalama wa wafanyakazi.
Kasoro nyingine
ni wakandarasi kufanya kazi zaidi ya viwango vya madaraja yao, miradi
kutosajiliwa na kutokuwa na mabango.
0 comments:
Post a Comment