*Yaingia DRC, yaua watu watatu, sita wagonjwa
*Mipango ya kukabiliana nao yaandaliwa Temeke
Hussein Ndubikile
Dk. Mpoki Ulisubisya |
SERIKALI imetoa hadhari kwa mikoa
inayopakana na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) baada ya kuzuka kwa
ugonjwa Ebola huku watu watatu wakipoteza maisha.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya
Shirika la Afya Duniani (WHO) kutangaza Mei 12 kuwapo mlipuko wa ugonjwa huo
kupitia vipimo vya maabara baada ya kugundulika wagonjwa tisa, kati yao watatu
wakifariki dunia huku wengine sita wakiendelea na matibabu katika kituo
kilichoandaliwa maalumu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya, alisema ugonjwa huo ulizuka katika jimbo la
Kaskazini Mashariki la Bas Uele huku akisisitiza kuwa hadi sasa nchini hakuna
mgonjwa aliyehisiwa kuwa na virusi vya Ebola.
“Nchi yetu inapakana na DRC, hivyo iko
hatarini kuambukizwa ugonjwa huu kutokana na mwingiliano wa watu hasa wanaotoka
na kuingia nchini, hadhari lazima ichukuliwe,” alisema Dk Ulisubisya.
Alisema wananchi wanaoishi mikoa ya
mipakani na nchi hiyo ikiwamo Mwanza, Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa na Songwe,
kuchukua hadhari na kushirikiana na Serikali ili ugonjwa huo usilete madhara.
Alisisitiza kuwa baada ya taarifa hizo,
Wizara imechukua hatua mbalimbali zikiwamo za utoaji mafunzo kwa watumishi ya
jinsi ya kuutambua na kuandaa mipangokazi ya kukabiliana nao.
Pia kupeleka vifaa kinga kwenye kituo
cha Temeke kwa wagonjwa wa Dar es Salaam, Pwani na Morogoro ili kuziwezesha
maabara za Taifa kutambua ugonjwa huo.
Nyingine ni utoaji taarifa ya hadhari
kupitia makatibu tawala na waganga wakuu wote wa mikoa, uitishaji wa mikutano
ya dharura wa uratibu wa kikosikazi cha Taifa, uundaji timu ya haraka
itakayokwenda mikoa jirani na nchi hiyo na kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji kwenye
vituo vya mipakani vikiwamo viwanja vya ndege na bandari kavu, kuendelea kutoa
elimu kwa jamii.
Aidha, alisema hadhari ya ugonjwa huo
haitaishia katika mikoa hiyo bali hata viwanja vikubwa vya ndege kikiwamo cha
Mwalimu Julius Nyerere.
Aliongeza kuwa Ebola huambukizwa kwa
njia ya kugusa damu au majimaji kutoka kwa mtu aliyeambukizwa, kugusa maiti,
kugusa wanyama wazima na walioambukizwa.
Alifafanua kuwa dalili za ugonjwa huo
huanza kuonekana kwa mtu aliyeambukiza baada ya siku mbili hadi 21 tangu kupata
maambukizi, homa ya ghafla, kulegea kwa mwili, maumivu ya misuli, kuumwa
kichwa, vidonda kooni, kutokwa damu ndani na nje ya mwili.
0 comments:
Post a Comment