Abraham Ntambara
SIKU moja baada ya Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Kata ya Bungu wilayani Kibiti, Alife Mtulia, kuuawa kwa kupigwa risasi na watu
wasiojulikana akiwa nyumbani kwake, imeelezwa kuwa wauaji hao waliacha ujumbe wakidai
marehemu alikuwa akidhulumu watu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga alisema
mauaji hayo yalifanyika usiku wa kuamkia jana, huku akiahidi kutoa ufafanuzi wa
kina leo.
Mauaji ya askari Polisi, viongozi wa Serikali za Mitaa na
raia yamekuwa yakifanyika mara kwa mara katika wilaya za Kibiti, Rufiji na
Mkuranga mkoani Pwani.
Jumanne wiki hii akiwasilisha bungeni bajeti ya wizara
yake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba aliliambia Bunge kuwa
Serikali itaanzisha mkoa mpya wa kipolisi katika wilaya za Kibiti, Rufiji,
Mkuranga na Mafia, ambao utaitwa mkoa wa kipolisi Rufiji.
“Mtulia aliuawa akiwa anaelekea bafuni kuoga. Walimvamia
wakampiga risasi na kupoteza maisha. Hili tukio limetokea kweli ameuawa. Ila
marehemu hakuwa katibu wa chama wa tawi,
alikuwa kiongozi miaka ya nyuma sielewi alistaafu lini,” alisema.
Alibainisha kuwa sababu za mauaji hayo hazijafahamiaka,
licha ya wauaji hao kuacha ujumbe wa maandishi.
“Katika ujumbe huo wauaji walidai kuwa marehemu alikuwa
mtu wa kudhurumu. Ila hawakusema alidhulumu lini na alimdhulumu nani,” alisema.
Alisema Jeshi la Polisi linaendelea na msako wa watu
waliofanya mauaji hayo, mpaka jana jioni hakuna mtu aliyekamatwa.
“Tunaendelea na msako. Nawataka tu wananchi kuwa watulivu
katika kipindi hichi ambacho tunaendelea kuwasaka wauaji,” alisema.
Hivi karibuni Jeshi la Polisi liliwaua watu wanne
wanaosadikiwa kuhusika na mauaji ya askari polisi wanane na uporaji wa silaha
katika eneo la Mkengeni, Kata ya Mjawa, Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani. Tukio
hilo lililotokea takribani wiki mbili zilizopita.
Jeshi hilo lilieleza chanzo cha mauaji ya askari polisi
kujirudia mara kwa mara katika maeneo hayo ya Mkuranga, Rufiji, Ikwiriri na
Kibiti kuwa ni eneo hilo kuzungukwa na pori.
Akizungumza kuhusu tukio hilo katika Makao Makuu ya
Polisi jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Nsato Mssanzya
alisema baada ya majambazi hao kuwaua askari hao walipora bunduki saba na
kutokomea kusikojulikana.
Alisema baada ya tukio hilo polisi walifanya operesheni
na kufanikiwa kutambua maficho ya muda ambapo katika majibizano ya risasi
walifanikiwa kuwaua watu hao wanne pamoja na kupata silaha nne mbili zikiwa ni
za askari waliouawa na mbili za majambazi hao.
0 comments:
Post a Comment