Suleiman Msuya
JUKWAA la Haki na Usalama limeainisha mambo
101 ambayo mwananchi anapaswa kuyajua kuhusu Polisi, huku ikitangaza mpango wa kugawa
vitabu 7,000 vilivyobeba ujumbe huo, ambapo 300 kati yao vitaelekezwa kwa watu
wenye mahitaji maalumu.
Mjumbe wa Baraza la Uongozi la Chama cha
Wanasheria Tanganyika (TLS), Madeline Kimei wakati akizindua na kukabidhi
vitabu 20 vya nukta nundu kwa shule ya msingi ya Uhuru Mchanganyiko, Ilala Dar
es Salaam jana, alitaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni uhuru wa majadiliano, uwajibikaji
na mipaka ya kazi ya Jeshi hilo.
Alisema TLS imejipanga kugawa vitabu
hivyo vitakavyosaidia jamii ambayo imekuwa ikikabiliwa na changamoto ikutanapo
na polisi.
Kimei alisema TLS kwa kushirikiana na Jukwaa
la Haki na Usalama imeandaa machapisho manne kuhusu polisi, mawili ni nyaraka
za majadiliano kuhusu uhuru wa kioperesheni na uwajibikaji wa Jeshi hilo.
Alisema mengine mawili ni vitabu vya
uelewa kwa wananchi juu ya polisi na mabaraza ya usalama ya wilaya, ambapo
mwitikio umekuwa mkubwa.
“Leo tuko hapa kuzindua toleo la
nuktanundu la mojawapo ya vitabu vilivyochapishwa chini ya mradi huu, na kitabu
hiki kinaitwa ‘Mambo 101 Unayohitaji Kufahamu Juu ya Polisi Lakini Unaogopa
Kuuliza’,” alisema.
Mjumbe huyo alisema uandaaji wa vitabu
vya nuktanundu una gharama kubwa, lakini kutokana na kutambua umuhimu wa kundi
hilo, walilazimika kuchapisha vitabu 300 kwa kuanzia katika kundi hilo.
Alisema lengo kuu ni kuhakikisha
wananchi wanatambua kazi za Polisi zinavyofanywa na changamoto wanazokutana
nazo.
Kimei alisema kitabu hicho kitaelimisha
jamii jinsi Jeshi hilo linavyofanya kazi na ukomo wake wa madaraka, hivyo kila
pande kutekeleza majukumu yake kwa haki.
Akizungumza baada ya uzinduzi huo, Ofisa
Elimu Maalumu wa Wilaya ya Ilala, Salehe Msechu alisema uamuzi wa Jukwaa la
Haki na Usalama ni wa kuungwa mkono na jamii, huku akisisitiza wadau wengine
kujitokeza kusaidia.
Msechu alisema Serikali imejipanga
kusaidia kundi la watu wenye mahitaji maalumu, hivyo itajitahidi kutoa vifaa
vitakavyotumika kwa wanafunzi wa wilaya hiyo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi
Mchanganyiko, Anna Msechu alisema shule hiyo ina wanafunzi 69 wasioona hivyo
vitabu hivyo vya nuktanundu vitasaidia kutatua tatizo.
“Hapa nina wanafunzi 69 watakaofaidika
na vitabu hivi; havikidhi mahitaji lakini vitasaidia kwa kiasi fulani, tunaomba
wadau wengine wajitokeze kusaidia,” alisema.
Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wasioona
Tanzania, Jonas Lubago alisema vitabu vya watu wa elimu maalumu hasa wasioona nchini
vinapatikana kwa chini ya asilimia moja, hivyo jitihada zinahitajika kukidhi mahitaji.
0 comments:
Post a Comment